DADA HOOD KUUNGA MKONO JUHUDI ZA RAIS SAMIA KUINUA MICHEZO YA WANAWAKE.
Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa kushirikiana na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Dada Hood inayojishughulisha na kupinga unyanyasaji wa kijinsia wameandaa Tamasha la kuichangia timu ya taifa wanawake ya mpira wa miguu (Twiga Stars).
Akizungumza na waandishi wa habari Februari 23, 2022 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa taasisi hiyo Mkuwe Issac (Mammy Baby) amesema tamasha hilo litafanyika Machi 8, 2022 wakati wa maadhimisho ya Siku ya wanawake Duniani jijini Dar es salaam.
"Siku hiyo tumeipanga kwa kazi tatu ambazo ni kufanya harambee kuichangia timu ya wanawake Twiga Stars, kuzindua albamu ya 'The Orange' na kuonesha vipaji vya wanawake katika tasnia muziki" amesema Mkuwe.
Aidha, Mkurugenzi huyo amesema taasisi yake inaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya 6 chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye sekta za Sanaa na Michezo.
Tamasha hilo litakalofanyika Siku ya Wanawake Duniani litapambwa na wasanii wa kike 10 ambapo wasanii wa kiume pia watakuwepo.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT)Neema Msitha amewapongeza Dada Hood kwa kazi zao za kuwainua watoto wa kike hasa nia yao ya kuichangia timu ya wanawake ya Taifa Twiga Stars.
Msitha ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi siku hiyo ili kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kusaidia sekta ya michezo kwa upande timu za taifa za wanawake ambazo zinaendelea kupeperusha vema bendera ya taifa kimataifa.
Naye Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Sanaa Bi Leah Kihimbi amesema Rais Samia Suluhu Hassan anapenda Sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo na taasisi ya Dada Hood ndiyo wamefungua milango ya mashirikiano na Serikali kwenye sekta ya Sanaa na Michezo na kuzitaka taasisi nyingine kuiga mfano huo kwa maslahi mapana ya taifa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Wanawake (TWFA) Somoe Ng'itu ameishukuru Serikali kwa kushirikiana na Taasisi ya Dada Hood na kutoa wito kwa wadau wengine kuendelea kuwashika mkono Twiga Stars ili waendelee kuliheshimisha taifa kimataifa.