Michezo kwa jamii

PROGRAMU YA MAFUNZO YA MICHEZO KWA JAMII

Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limekuwa likiratibu mafunzo ya michezo kwa jamii kama sehemu ya kuwajengea uwezo walimu na makocha wa michezo mbalimbali ili waweze kutumia ujuzi huo kuwafundisha wanamichezo wa michezo mbalimbali.

Lengo la mafunzo hayo ni kuwaongezea ujuzi wa kitaalam walimu na makocha wa michezo mbalimbali na kuwaongezea ubunifu wa kutumia rasilimali zilizopo katika maeneo yao kwa ajili ya kufundisha michezo kwenye jamii.

Mafunzo haya yanalenga kufundisha makocha na walimu wa michezo yote katika shule za msingi na sekondari na kwa michezo ile ya kipaumbele ambayo ni Soka, Netiboli, Riadha, Wavu, Kikapu na Ngumi.

Programu hii endelevu kwani BMT inaamini kuwa michezo ni sayansi inayobadilika mara kwa mara katika ufundishaji, hivyo itaendelea kutoa mafunzo haya kila wakati pale inapohitajika na uwezo wa uwezeshaji yaani bajeti ikiwepo.

Programu hii imesaidia kuendeleza ujuzi na maarifa kwa walimu na makocha wa michezo hivyo kuzalisha wanamichezo hodari katika michezo kama vile soka, riadha, kuogelea na tenisi.

Mpango huu unatambulika na Serikali kupitia BMT ambayo imekuwa ikishirikiana na mashirikisho ya michezo ya kitaifa na vyama vya michezo vya kitaifa katika kuratibu na kutoa wakufunzi. BMT imekuwa ikiwezesha mpango huu kupitia bajeti yake ya kila mwaka.

Mpango huu upo chini ya mpango wa baraza la michezo la taifa sambamba na mpango wa taifa wa kuhakikisha tunahamasisha makocha wa michezo mbalimbali kushiriki mafunzo kwa ajili ya kuongeza uwezo wa ufundishaji wa michezo nchini.