Mradi wa Utawala Bora
PROGRAMU YA UENDELEZAJI UTAWALA BORA KATIKA VYAMA NA MASHIRIKISHO YA MICHEZO
- Utangulizi
Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa mujibu wa Sheria Na.49 lina jukumu la kuratibu, kusimamia na kuthibiti aina zote za michezo kwa kushirikiana na vyama na mashirikisho ya michezo kitaifa. Hivyo, Baraza katika kutekeleza mpango kazi wake limekuwa likiendelea kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha utawala bora, uwazi na uwajibikaji katika kusimamia shughuli za Vyama na Mashirikisho ya Michezo. Lengo ni kuhakikisha vyama vinaendeshwa kwa kuzingatia misingi ya kitaifa na kimataifa ya uendeshaji wa michezo.
- Usimamizi wa Kisheria na Uzingatiaji wa Katiba
Baraza la Michezo la Taifa katika kutekeleza jukumu la usimamizi wa vyama na mashirikisho linahakikisha kila chama cha michezo kimesajiliwa kwa mujibu wa Sheria na kina katiba inayozingatia misingi ya utawala bora, uwazi, uwajibikaji na demokrasia.
- Ufuatiliaji wa Uongozi na Usimamizi wa Uchaguzi
Baraza la Michezo la Taifa limekuwa likisimamia kwa ukaribu mikutano mikuu ya viongozi wa vyama/mashirikisho pamoja na mikutano ya uchaguzi wa viongozi ili kuhakikisha chaguzi zinaendeshwa kwa njia ya haki na demokrasia.
Vilevile, Baraza limekuwa likizuia migongano ya maslahi na uongozi wa muda mrefu usiozingatia katiba ya Chama na Shirikisho la mchezo husika. Pia, Baraza linawataka vyama kuwasilisha taarifa za utendaji kazi na kuwasilisha taarifa za mapato na matumzi ya fedha iliokaguliwa na kuwasisitiza kuwa fedha za michezo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
- Ujenzi wa Uwezo (Capacity Building)
Baraza lina jukumu la kuratibu mafunzo ya utawala bora kwa viongozi wa vyama vya michezo na pia kuwapa miongozo ya utawala bora kwa lengo la kuwajengea uwezo viongozi wa vyama vya michezo na mashirikisho ya michezo hapa nchini. Pia, Baraza linaelimisha Vyama kuhusu maadili ya michezo na kanuni za kimataifa.
- Utatuzi wa Migogoro
Baraza linajukumu la kupokea na kushughulikia migogoro ya kiuongozi na kikatiba ya vyama vya michezo. Pia Baraza linatoa ushauri na kuwaelekeza vyama kutumia vyombo sahihi vya haki za michezo ambazo ni kamati za maadili, rufaa na nyinginezo.
- Utekelezaji wa Maadili na Nidhamu
Baraza linafanya jukumu la kusimamia utekelezaji wa kanuni za maadili, sera kupinga rushwa, unyanyasaji wa kijinsia, upangaji wa matokeo na kupinga matuimizi ya dawa na mbinu haramu michezoni (corruption, sexual harassment and abuse, match fixing and doping). Pia, Baraza linaelekeza vyama kuwa na kanuni za maadali, kuepuka mgongano wa kimaslahi na kuvumiliana. Vilevile Baraza huchukua hatua pale chama / Shirikisho liinapokiuka misingi ya utawala bora kwa kutoa onyo, kusimamisha misaada na kusimamisha katika nafasi za uongozi.
- Ulinganifu na Viwango vya Kitaifa na Kimataifa
Baraza lina jukumu la kuhakikisha vyama vinaendeshwa kwa kuzingatia Sera ya maendeleo ya michezo na matakwa ya Sheria ya nchi. Pia kupitia mikataba na miongozo ya mashirikisho ya michezo kimataifa ili kuhakikisha maslahi mapana ya michezo nchini.
- Faida za Kuzingatia Utawala Bora
- Kuboresha utendaji na kupata matokeo chanya.
- Huvutia ufadhili na kujenga uaminifu na ushirikiano na wadau wengine
- Huzuia au kupunguza migogoro na kashfa
- Kuhakikisha maendeleo ya muda mrefu katika michezo.
- Hitimisho
Kwa ujumla, utekelezaji wa utawala bora umechangia kuimarika kwa ufanisi wa uendeshaji wa chama, kuongeza uwajibikaji wa viongozi na kuweka msingi imara wa maendeleo endelevu ya michezo. Kwa kufanya hivyo Vyama vya michezo vinaendelea kushirikiana na Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa na wadau wengine na kuhakikisha viwango vya juu vya utawala bora vinaendelezwa kwa maslahi mapana ya michezo nchini.

