Tuzo za Wachezaji Bora wa Kitaifa

PROGRAMU YA UTOAJI WA TUZO ZA WANAMICHEZO BORA WA MWAKA

 

1.0 Utangulizi

Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limekuwa na jukumu la msingi la kukuza na kuendeleza michezo kwa kushirikiana na vyama na mashirikisho ya michezo ya kitaifa nchini. Baraza limekuwa na mikakati mbalimbali ya kuchochea maendeleo ya michezo mojawapo ya mkakati wa Baraza ni utoaji wa tuzo za wanamichezo wanaofanya vizuri kwa kila mwaka kwenye mashindano ya michezo mbalimbali ya kitaifa

 

2.0 Lengo

Baraza limeweza kUratibu utoaji wa tuzo kwa wanamichezo waliofanya vizuri kwa misimu mitatu mfululizo ili kusherekea mafanikio ya timu na wanamichezo wetu katika mashindano ya kimataifa na kitaifa. Tuzo hizo zimetumika kama kichocheo kikubwa cha mafanikio haya makubwa yanayoonekana katika sekta ya michezo nchini.

 

2.1 Malengo Mahsusi ya Tuzo

  • Kutambua na kusherekea ubora na mafanikio ya wanamichezo katika mashindano ya kimataifa
  • Kuhamasisha ushiriki wa jamii katika michezo na kuifanya sekta ya michezo kuonekana sekta muhimu ya kiuchumi
  • Kukuza ushiriki wa jamii katika Jumuiya zote za kitaifa za michezo na mashirikisho kupitia mashindano
  • Kutoa fursa kwa wadau mbalimbali wa michezo kufahamiana pamoja na kubadilishana mawazo juu ya masuala mbalimbali ya michezo

 

3.0 Uratibu na Usimamizi wa Tuzo

Shughuli hii ya utoaji wa tuzo inaratibiwa na kusimamiwa na;  

  • Kamati ya Usimamizi wa Tuzo za Michezo yenye wajumbe tisa (9) ambao waliteuliwa na Baraza la Michezo la Taifa.
  • Sekretarieti: Inayoundwa na watumishi wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ambao wanakuwa na jukumu la usaidizi na utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya kamati ya usimamizi wa tuzo za michezo
  • Kampuni ya uratibu wa matukio ya michezo ambapo Baraza limekuwa likitumia kampuni kwa ajili ya kuufanya usiku wa wanamichezo kuwa tukio la kukumbukwa.

 

4.0 Vipengele vya Tuzo

Baraza limekuwa likifanya kazi kwa ukaribu sana na Vyama na mashirikisho ya michezo ya kitaifa katika kuwatambua wanamichezo na timu zilizofanya vizuri katika tasnia ya michezo. Vyama/mashirikisho vinaandikiwa barua na kupewa fomu maalumu ili kuwasilisha majina ya wachezaji, viongozi, wataalaumu na timu zilizofanya vizuri na kupitiwa na Sekretarieti na baadaye kuthibitishwa na Kamati ya usimamizi. Vipengele vya tuzo ni kama ifuatavyo;

  1. Mwanamichezo Bora wa Kiume
  2. Mwanamichezo Bora wa Kike
  3. Mwanamichezo Bora Kijana wa Kiume
  4. Mwanamichezo Bora Kijana wa Kike
  5. Mwanamichezo Bora wa Kiume mwenye Ulemavu
  6. Mwanamichezo Bora wa Kike mwenye Ulemavu
  7. Timu Bora ya Mwaka ya Wanaume
  8. Timu Bora ya Mwaka ya Wanawake
  9. Kiongozi Bora wa Michezo wa Kiume wa Mwaka
  10. Kiongozi Bora wa Michezo wa Kike wa Mwaka
  11. Kocha Bora wa Kiume wa Mwaka
  12. Kocha Bora wa Kike wa Mwaka
  13. Mwanamichezo Bora wa kiume/Kike kutoka Shuleni (UMITASHUMTA na UMISSETA)
  14. Mwamuzi Bora wa Kiume wa Mwaka
  15. Mwamuzi Bora wa Kike wa Mwaka
  16. Mwanahabari za Michezo Bora wa Kiume wa Mwaka
  17. Mwanahabari za Michezo Bora wa Kike wa Mwaka
  18. Tuzo ya Uchaguzi wa watu ‘People’s Choice Awards (Mwanaume)
  19. Tuzo ya Uchaguzi wa watu ‘People’s Choice Awards ( Mwanamke)

 

5.0 Faida za Tuzo

  • Wanamichezo waliofanya vizuri wanapata nafasi ya kupongezwa na kuenziwa na Serikali kupitia Baraza kwa kutoa mchango wao mkubwa kwenye michezo, ikiwa ni ishara ya heshima na kutambuliwa kwa kazi zao za michezo katika mashindano mbalimbali ya kimataifa
  • Kutoa motisha na hamasa ya kufanya vizuri zaidi; tuzo hizo zimekuwa zikitoa hamasa na msukumo kwa wachezaji kuendelea kufanya vizuri na kuongeza juhudi katika mazoezi na mashindano
  • Kukuza viwango vya michezo nchini kwa kuwapongeza wanamichezo bora, tuzo hizo zimekuwa zikiongeza ushindani na viwango vya utendaji na kuibua maarifa mapya kwa wachezaji
  • Kuibua hadhi na utambulisho wa Tanzania kupitia wanamichezo waliofanya vizuri kimataifa
  • Kuibua na kuchochea kujifunza michezo kwa vijana na watoto kwa kuwa tuzo hizi utangazwa katika mitandao ya kijamii hivyo vijana wanapata nafasi ya kujua hata aina ya michezo nchini kwa kuona kwa vitendo jinsi ya wanamichezo hao wanavyopewa zawadi mbalimbali zikiwamo kupewa Zawadi ya ‘trophy’ na pesa taslimu.

 

6.0 Tarehe ya Utoaji Tuzo na Mgeni Rasmi

Kamati wa usimamizi na uratibu wa utoaji tuzo za wanamichezo bora upanga tarehe ya tukio, ambayo huwa usiku na mmoja ambapo wanamichezo wote waliopendekezwa na kamati wanakutana na kusherekea siku hiyo kwa namna ya kipekee. Pia wageni mbalimbali wa Serikali na taasisi za michezo hualikwa kujumuika pamoja kusherekea usiku wa tuzo za wanamichezo bora. Kamati upendekeza jina la mgeni rasmi kutoka Serikalini.

 

7.0 WAGHARAMIAJI WA TUZO, NA WAFADHILI

Shughuli ya tuzo kwa wanamichezo bora imekuwa ikigharamiwa na Serikali kwa kushirikiana, wafadhili na wadhamini mbalimbali.