Maandalizi ya Afcon 2027
Utangulizi
AFCON ni Mashindano ya Mpira wa Miguu kwa Mataifa ya Afrika. Mashindanpo hayo yalianzishwa mwaka 1957. Tangu kuanzishwa hadi kufikia mwaka 2026 ni takribani miaka 69 imepita na yamejizolea umaarufu mkubwa barani Afrika na duniani kote. Tangu kuanzishwa, Tanzania imefanikiwa kushiriki mara nne (4) ambayo ni mwaka 1980 yaliyofanyika nchini Nigeria, 2019 nchini Misri, 2023 nchini Ivory Coast na 2025 nchini Morocco. Katika mwaka 2025, Tanzania ilifanikiwa kuvuka hatua ya makundi na kufikia hatua ya 16 bora. Mwaka 2027 mashindano hayo yamepangwa kufanyika katika nchi za Afrika Mashariki kwa maana ya Tanzania, Kenya na Uganda.
Tanzania, Kenya na Uganda kupitia Pamoja Bid zilishinda zabuni ya kuwa wenyeji wa mashindano ya AFCON 2027. Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa mashindano hayo kufanyika katika nchi za Afrika Mashariki tangu kuanzishwa kwake. Baada ya ushindi wa zabuni ya kuandaa, mataifa yote matatu (3) yalielekezwa kuboresha miundombinu ili kukidhi vigezo vinavyokubalika kimataifa kuweza kuwa wenyeji wa mashindano hayo. Miundombinu hiyo inahusisha viwanja vya mashindano, viwanja vya mazoezi, miundombinu ya usafiri kutoka na kuelekea viwanjani na huduma za msingi za kijamii kwa timu na mashabiki zikiwemo sehemu za malazi yaani hoteli.
Ili kufanikisha maandalizi, kila nchi ilielekezwa kuwa na vituo vitatu vya mashindano huku kila kituo kikitakiwa kuwa na viwanja vitano vya mazoezi vyenye ubora ambavyo vitatumiwa na timu shiriki. Kwa upande wa Tanzania, vituo vya mashindano vitakuwa ni; uwanja wa Benjamin Mkapa – Dar es Salaam, Uwanja wa Fumba - Zanzibar na uwanja wa Arusha uliopo jiji Arusha.
Ili kupima uwezo na utayari wa mataifa hayo kuwa wenyeji wa AFCON 2027, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) liliandaa mashindano ya CHAN 2024 katika nchi wenyeji ambayo yalifanyika kuanzia tarehe 02 – 30 Agosti, 2025 ikiwa ni kipimo cha utayari huo.
Kwa upande wa Tanzania, vituo vya mashindano ya CHAN 2024 vilikuwa ni uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na Aman, Zanzibar. Mashindano hayo yalifanyika kwa mafanikio makubwa hali iliyomlazimu Rais wa CAF kutoa tuzo za heshima kwa wakuu wa nchi hizi tatu (3) tarehe 19 Novemba, 2025 nchini Morocco.
1.4.2 Hatua Zilizofikiwa Kuelekea AFCON 2027
Kufuatia ushindi wa zabuni ya kuandaa mashindano hayo, Serikali ilianza ujenzi wa Uwanja mpya wa Arusha, viwanja vya mazoezi na ukarabati wa uwanja wa Benjamin Mkapa na kwa upande wa Zanzibar ujenzi wa uwanja mpya wa fumba na viwanja vya mazoezi umeanza kwa kuzingatia maelekezo ya CAF. Hadi sasa utekelezaji wa miradi hiyo unaendelea vizuri na unatarajiwa kukamilika kwa muda uliopangwa. Aidha, katika hatua nyingine Serikali iliunda Kamati ya Kitaifa, Wataalam na ya Ndani (Local Organizing Commitee). Pia, maandalizi yote kwa maana ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya michezo yapo katika hatua nzuri za utekelezaji.

