MWONGOZO WA KUSAIDIA TIMU ZA TAIFA KUSHIRIKI MICHEZO KITAIFA NA KIMATAIFA

Utangulizi

Serikali kupitia Wizara yenye dhamana ya Michezo na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), imeamua kuendeleza juhudi za kuhakikisha timu za Taifa zinafanya vizuri katika michezo na mashindano ya kitaifa na kimataifa . Juhudi hizi zinahusisha ufuatiliaji wa rasilimali fedha za kugharamia maandalizi na ushiriki katika mashindano ya kitaifa na kimataifa  kwa kushirikiana na Vyama/ mashirikisho ya michezo, wadau mbalimbali, kamati za michezo na washirika  wa maendeleo ya michezo. 

Sababu ya Kuwepo Mwongozo

Mwongozo huu utaimarisha mwenendo wa kusaidia timu za taifa , ambapo unaweka msingi madhubuti ya chama. Shirikisho kuwa na mipango ya maendeleo na kuwa na utaratibu mzuri wa kupata timu ya taifa ili waweze kunufaika  na fursa  hii.

Maeneo ya Mwongozo

Mwongozo huu unaweka utaratibu wa namna ambayo Serikali itazihudumia timu za taifa kwa kushirikiana na vyama/mashirikisho  na wadau mbalimbali wa michezo nchini. Mwongozo huu umeainisha vigezo vya awali vinavyohitajika kwa timu ya Taifa au Chama/Shirikisho kupata usaidizi wa timu ya Taifa . Eneo la kwanza linahusiana na  utawala bora kwa vyama na mashirikisho husika na eneo la pili ni vigezo vya mchezo husika kimatifa ambavyo huitajika kuwa vimekidhiwa kabla ya kushiriki mashindano ya mchezo huo. 

Vigezo vya Kufuata

  1. Vigezo vya kuzingatia katika kusaidia timu za Taifa hasa katika maandalizi na mashindano ya kimataifa yanategemea uwezo wa Serikali , Vyama/ Mashirikisho husika na wadau wengine kama ifuatavyo;
  2. Timu ya Taifa itakayonufaika lazima iwe inasimamiwa na chama/ shirikisho ambalo limesajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa. Aidha, chama hicho kinapaswa kukidhi vigezo vingine muhimu ambavyo ni;-
  3. Chama cha Taifa lazima kiwe na sura ya kitaifa hivyo kiwe na uwakilishi wa zaidi ya 50% ya Mikoa yote nchini,  isipokuwa kwa Michezo ya Watu  yenye Ulemavu na baadhi ya michezo yenye asili ya Sanaa za mapigano na michezo au vyama vipya.
  4. Chama kifuate katiba ya Chama/ Shirikisho husika katika utekelezaji wa shughuli zake;
  5. Chama/Shirikisho kuendesha shughuli zake kwa kuzingatia misingi ya utawala bora ikiwemo, uwazi, uwajibikaji, demokrasia na ushirikishaji;
  6. Chama/shirikisho liwe linalipa ada ya kila mwaka za (BMT) na kusimamia wanachama wake wote kulipa ada  ili wawe hai wakati wote kushiriki shughuli za chama/shirikisho lao;
  7. Chama/Shirikisho kiwe kinafuata kanuni na miongozo yote inayotolewa na Serikali juu ya uendeshwaji wa michezo nchini;
  8. Chama /Shirikisho kuwa na mahesabu ya fedha yaliyokaguliwa na taasisi inayotambulika kisheria kila mwaka.
  9. Timu ya Taifa ambayo imefuzu au ina sifa mahsusi za kushiriki mashindano
  10. makubwa ya kimataifa kama vile; Olimpiki kawaida na Olimpiki maalumu, Paralimpiki, Jumuiya ya Madola, Michezo ya Mataifa ya Afrika (All Africa Games), Mashindano ya Afrika Mashariki, Mashindano ya Kanda za Afrika, Mashindano ya Afrika na ya Dunia, hii itahusisha michezo ya mtu mmoja mmoja na michezo ya timu kwa ujumla. 
  11. Timu ya taifa itasaidiwa kwa kuangalia manufaa na tija ya mashindano husika kama yana faida kwa nchi na maendeleo ya mchezo wenyewe. Mfano kama yana tija kiuchumi, kijamii na mahusiano ya kidiplomasia.     
  12. Timu ya taifa itapewa kipaumbele cha kusaidiwa kama mashindano wanayoshiriki yapo kwenye kalenda yao ya chama/shirikisho ya mwaka iliyowasilishwa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa mwaka husika. Mashindano yasiyokuwepo katika kalenda yatazingatiwa endapo zipo sababu za kutosha kufanya hivyo na kama vigezo vingine vyote vimekidhi.
  13. Timu ya Taifa itasaidiwa kwa kuangalia mpango endelevu (Sustainability) wa Chama/Shirikisho walionao juu ya timu hiyo, kama vile uwepo wa programu za maendeleo za mafunzo/ufundi, mashindano, kutafuta rasilimali fedha, miundombinu na vifaa ili kupanua wigo wa wanachama, uwepo wa mpango mkakati na uwepo wa mpango kazi.
  14. Michezo iliyoainishwa katika mkakati wa taifa kuwa ni kipaumbele itazingatiwa zaidi katika kusaidia timu zake za taifa ikitekelezwa sambamba na vigezo vingine vyote vilivyomo katika mwongozo huu.
  15. Timu ya taifa iliyoundwa kwa kuzingatia misingi na utaratibu sahihi wa uundaji wa timu za Taifa kwa kuzingatia mwongozo wa uteuzi wa timu za Taifa wa Chama/Shirikisho husika utakaoridhiwa na serikali.
  16. Uwezo wa chama kutafuta, kuchangia gharama na kusimamia matumizi ya   fedha kwa mujibu wa sheria.
  17. Timu ya taifa iwe chini ya Chama/Shirikisho lenye mahusiano mazuri na
  18. Vyama/Mashirikisho mengine ya michezo ya kitaifa na kimataifa na baina ya wadau na washirika wengine wa michezo.
  19. Chama/ Shirikisho linalohakikisha  mashindano ya ndani yanayofanyika.

 

Utaratibu wa Maombi

Chama/Shirikisho, litapaswa kutuma maombi kwa kuandika barua kwenda kwa: Katibu Mtendaji, Baraza la Michezo la Taifa S.L.P. 20116, DSM.  Maombi yanaweza kutumwa kwa njia ya Posta, au kwa barua pepe ya Baraza ambayo ni info@nationalsportscouncil.go.tz. Barua hiyo iainishe mambo yafuatayo;

  1. Aina ya mashindano.
  2. Ratiba ya mashindano.
  3. Bajeti ya kuandaa/kushiriki mashindano hayo.
  4. Mpango kazi wa maandalizi na ushiriki wa timu ya taifa.
  5. Timu ya Taifa iliyoteuliwa.
  6. Uthibitisho wa uhai wa chama/shirikisho katika taasisi za kitaifa na  kimataifa anazojishirikisha nazo.
  7. Uthibitisho wa kufuzu au sifa za kushiriki mashindano husika.
  8. Uthibitisho wa taarifa ya mahesabu ya fedha yaliyokaguliwa kwa mujibu wa sheria.
  9. Maombi yawasilishwe Baraza la michezo la Taifa ndani ya muda usiopungua mwezi mmoja (1) kabla ya tarehe ya programu, tukio au mashindano husika yanayoombewa uwezeshaji.

HITIMISHO

Timu za Taifa chini ya usimamizi wa Vyama/Mashirikisho yatapaswa kuwa na vyanzo endelevu vya kutafuta rasilimali fedha za kugharamia shughuli za michezo na kuhakikisha inatumia msaada wa Serikali kuongezea nguvu ya kutekeleza maandalizi na mashindano ya ushiriki wa timu kimataifa kwa ufanisi zaidi. Pia kutumia vizuri fursa zinazopatikana kutoka mashirikisho ya kimataifa.