MPANGO WA KUWEZESHA TIMU ZA TAIFA KUSHIRIKI KATIKA MASHINDANO YA KIMATAIFA

  1. Utangulizi

Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa mujibu wa Sheria Na.49 lina jukumu la kuwezesha Timu za Taifa zinaposhiriki mashindano mbalimbali. Ili kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi, Serikali kupitia Wizara yenye dhamana ya michezo na Baraza la Michezo la Taifa iliunda mfuko maalum wa maendeleo ya michezo uliopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa mkutano wa Bajeti ya mwaka 2021/2022.

Lengo kuu la mfuko huo ni kugharamia shughuli mbalimbali za maendeleo ya michezo ikiwa ni pamoja na kugharamia maandalizi na ushiriki mzuri wa timu za Taifa za michezo mbalimbali zinaposhiriki mashindano ya kimataifa.

 

Sifa ya Timu Itakayowezeshwa

  1. Timu ya Taifa itakayonufaika katika mpango huu ni lazima iwe inasimamiwa na Chama/ Shirikisho ambalo limesajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa. Aidha, chama hicho kinapaswa kukidhi vigezo vingine muhimu ikiwamo;
  • Chama/Shirikisho  lenye sura ya uwakilishi kitaifa
  • Chama/shirikisho linaloendesha shughuli zake kwa kuzingatia misingi ya utawala bora, uwazi, uwajibikaji na ushirikishaji
  • Chama/shirikisho hai linalolipa ada kila mwaka ya Baraza la
  • Michezo la Taifa (BMT) na kusimamia wanachama wake wote kulipa ili wawe hai wakati wote na kushiriki shughuli za chama/shirikisho
  • Chama /Shirikisho lenye hesabu za fedha zilizokaguliwa.

 

  1. Timu ya Taifa ambayo imefuzu au ina sifa mahsusi za kushiriki mashindano makubwa ya kimataifa kama vile Olimpiki na Olimpiki Maalum, Jumuia ya Madola, Mashindano ya Dunia, Michezo ya Mataifa ya Afrika (Africa Games), Mashindano ya kanda za Afrika, hii inahusisha michezo ya mtu mmoja mmoja na michezo ya timu kwa ujumla inayowakilisha taifa.
  1. Timu ya taifa inawezeshwa kwa kuangalia manufaa na tija ya mashindano husika kama yana faida kwa nchi na maendeleo ya mchezo wenyewe.
  2. Timu ya taifa itapewa kipaumbele cha kusaidiwa kama mashindano wanayoshiriki yapo kwenye kalenda yao ya Chama/Shirikisho ya mwaka iliyowasilishwa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa mwaka husika.
  3. Timu ya Taifa itasaidiwa kwa kuangalia mpango endelevu (Sustainability) wa Chama/Shirikisho walionao juu ya timu hiyo, kama vile uwepo wa program za maendeleo za mafunzo/ ufundi, kutafuta rasilimali fedha/miundombinu na vifaa ili kupanua wigo wa wanachama, mpango mkakati na uwepo wa mpango kazi.
  4. Michezo iliyoainishwa katika mkakati wa taifa kuwa ni kipaumbele itazingatiwa zaidi katika kusaidia timu zake za taifa ikitekelezwa sambamba na vigezo vingine vyote.
  5. Timu ya taifa iliyoundwa kwa kuzingatia misingi na utaratibu sahihi wa uundaji wa timu za Taifa. (Kuzingatia mwongozo wa uteuzi wa timu ya Taifa wa Chama/Shirikisho husika ulioridhiwa
  6. Uwezo wa chama kutafuta/kuchangia gharama na kusimamia matumizi ya   fedha kwa mujibu wa Katiba.
  7. Timu ya taifa iwe chini ya Chama/Shirikisho lenye mahusiano mazuri na yama/mashirikisho mengine ya michezo ya kitaifa na Kimataifa na baina ya wadau na washirika wengine wa michezo.

 

Mafanikio

Kupitia mpango huu wa kuwezesha timu za Taifa mafanikio mbalimbali yamepatika ikiwemo;-

  1. Ushindani wa timu za taifa katika mashindano ya kimataifa umeongezeka kama vile mpira wa miguu, riadha, ngumi, kriketi n.k.
  2. Viwango vya wachezaji vimeongezeka kupitia kambi na ushiriki wa mashindano ya mara kwa mara.
  3. Vipaji vipya vimeibuliwa na kuendelezwa kupitia ujumuishwaji katika timu za Taifa.
  4. Taswira ya Taifa kimataifa imeimarika kwa kuitangaza nchi kupitia micheazo.
  5. Kupata furasa zaidi ya kushiriki mashindano makubwa kama vile AFCON, Olimpiki, Michezo ya Jumuiya ya Madola,  michezo ya Afrika nk
  6. Kuongeza chachu ya ajira kwa vijana kupitia fursa ya kuwa makocha, waamuzi, wachezaji, madaktari nk).
  7. Hamasa kwa vijana katika ushiriki wa michezo imeogezeka vijana wengi wamekuwa na mwitikio mkubwa.