Wizara ya Maliasili Yaibuka Kidedea Mchezo wa Drafti SHIMIWI 2025
service image
15 Sep, 2025

Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kufanya vizuri katika medani ya michezo kwa kuibuka kidedea katika mchezo wa drafti kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo la Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) 2025 yanayoendelea kufanyika jijini Mwanza.

Timu hiyo ilifanikiwa kutwaa ushindi muhimu wa mabao 2– 0 dhidi ya Wizara ya Uwekezaji katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu.

Akizungumza mara baada ya ushindi huo, Bw. Gervas Mwashimaha ambaye ni mchezaji wa timu hiyo na Mwenyekiti wa Maliasili Sports Club, amesema ushindi huo umetokana na mazoezi ya muda mrefu na dhamira ya kuipatia Wizara heshima katika mashindano ya mwaka huu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi wa Mashindano ya SHIMIWI 2025, Appolo Kayungi, amezipongeza timu zote zilizoshiriki mchezo wa drafti kwa kuonesha nidhamu ya hali ya juu na ushindani uliojaa heshima na moyo wa michezo.

"Nizipongeze timu zote. Mmeonyesha nidhamu ya hali ya juu tangu mwanzo hadi mwisho wa mashindano haya. Hili ni jambo la kuigwa," amesema Kayungi.

Aidha, amewahimiza wanamichezo kuendelea kushiriki mashindano hayo kila mwaka kama sehemu ya kuimarisha afya kupitia michezo.

Hata hivyo, katika michezo mingine iliyochezwa Septemba 14, 2025, Timu ya netiboli ya Wizara ya Maliasili na Utalii haikuweza kufurukuta mbele ya timu ya Wizara ya Utumishi na kukubali kichapo cha magoli 71–19, hivyo kumaliza mashindano hayo katika nafasi ya nne.

Hadi sasa, Wizara ya Maliasili na Utalii imefanikiwa kujikusanyia kikombe kimoja kupitia mchezo wa drafti pamoja na medali mbili zilizopatikana kwenye mbio za mita 3000, mita 200 na draft mafanikio yanayodhihirisha kuwa sekta ya maliasili si tu nguzo ya uchumi na utalii, bali pia imejikita katika kukuza vipaji vya michezo miongoni mwa watumishi wake.