BMT KUENDELEA KUSIMAMIA MICHEZO AINA YOTE
Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limesema kuwa litaendelea kusimamia michezo yote nchini kama sehemu ya dhamira yake ya kuinua, kukuza na kuendeleza sekta ya michezo Tanzania.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Michezo Mwandamizi, Charles Maguzu, wakati akikabidhi bendera kwa timu ya taifa ya mchezo wa kutunisha misuli, katika hafla iliyofanyika Desemba 3, 2025 kwenye ukumbi wa Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam. Timu hiyo inatarajiwa kushiriki Mashindano ya Dunia yatakayofanyika Afrika Kusini tarehe 6 Desemba 2025, yakihusisha mataifa zaidi ya kumi.
Tanzania itawakilishwa na wachezaji watatu ambao ni Martha Mabula, Noah Schembe pamoja na Obadia Mwampeta.
Maguzu amewataka wadau wa michezo kuungana na BMT katika kuupa nguvu mchezo huo, akisema hatua hiyo itasaidia kuendeleza michezo nchini na kuitangaza Tanzania kimataifa.
Kwa upande wake, Nahodha wa timu, Martha Mabula, amesema maandalizi waliyofanya yanawapa imani kuwa watafanya vizuri na kulinda heshima ya taifa.
"Binafsi nimejipanga vizuri katika kipengele cha wanawake. Maandalizi yote yamekamilika na tunashukuru BMT kwa kutusimamia kwa hali na mali. Tumejipanga kupambana na kufanya vizuri," amesema.

