BARAZA LA MICHEZO LA TAIFA (BMT) NA UBALOZI WA JAPANI KUENDELEZA PROGRAMU YA KUBADILISHANA WATAALAMU (JAPAN EXCHANGE AND TEACHING PROGRAM
Baraza la Michezo la Taifa (BMT) leo tarehe 28 Januari, 2026 limekutana na wawakilishi wa Ubalozi wa Japani nchini Tanzania kwa lengo la kujadili maendeleo ya programu ya kubadilishana wataalamu ya JET (Japan Exchange and Teaching Program).
Lengo la kikao hicho lilikuwa kujadili namna ya upatikanaji wa wataalamu hao kutoka Tanzania ambao wataenda kutoa mafunzo ya mchezo wa Riadha katika mji wa Nagai nchini Japani. Hatua hii inalenga kuimarisha mahusiano yaliyopo na Japani katika sekta ya Michezo.
Katika kikao hicho, Baraza la Michezo la Taifa liliwakilishwa na Meneja wa Maendeleo ya Michezo, Bw. Benson Chacha. Upande wa Ubalozi wa Japan uliwakilishwa na Bi. Yoshino Shibata, Afisa Ubalozi kutoka Kitengo cha Siasa, Uhusiano wa Umma na Utamaduni, akisaidiwa na Bw. Festo Mulinda, Mshauri wa Siasa, Uhusiano wa Umma na Utamaduni.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Maafisa wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambao ni Afisa Michezo Mwandamizi Bw. Mohamed Mwinduchi, pamoja na Bi. Juliana S. Onyando, Mfiziotherapia Mwandamizi wa Wizara.

