BMT KUJA NA MSIMU WA NNE WA TUZO ZA BARAZA LA MICHEZO LA TAIFA
Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kupitia Kamati ya Usimamizi wa Tuzo za Baraza la Michezo la Taifa 'National Sports Council Awards' (NSCA), chini ya Mwenyekiti wake Prof. Mkumbukwa Madundo Mtambo, leo tarehe 03 Machi, 2026 imekutana katika ukumbi wa uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuanza maandalizi ya msimu wa nne wa tuzo hizo, zinazotarajiwa kufanyika mwanzoni mwa mwezi Mei 2026.
Tuzo za NSCA zinafanyika kwa mara ya nne mfululizo, kufuatia mafanikio makubwa ya awamu zilizopita zilizofanyika mwaka 2022, 2023 na 2024. Katika misimu hiyo, zaidi ya wadau 1,000 wa michezo walishiriki, wakiwemo wachezaji wa zamani na wa sasa, viongozi wa michezo, viongozi wa taasisi za Serikali na binafsi, wanahabari wa michezo, wafadhili pamoja na wadau mbalimbali huku maelfu ya Watanzania wakifuatilia tukio hilo kupitia vyombo vya habari.
Tuzo hizi zimeendelea kuwa chachu ya mafanikio kwa wanamichezo wetu kwa kuongeza ari, motisha na ushindani chanya, hususan katika mashindano ya kitaifa na kimataifa. Aidha, zimechangia kuhamasisha jamii kutambua na kuthamini mafanikio yanayopatikana katika sekta ya michezo nchini.
BMT imejipanga kuhakikisha msimu wa nne wa tuzo hizi unakuwa mkubwa zaidi, bora zaidi na wenye kuleta hamasa mpya kwa wadau wote wa michezo nchini.

