MSITHA AELEZA MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIWA NA VIONGOZI WA VYAMA VYA MICHEZO

KATIBU Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Neema Msitha, amevitaka vyama/mashirikisho na kamati za michezo nchini kufanya Kazi zao kwa kuzingatia misingi ya katiba zao.
Hayo ameyasema leo Mei 27, 2022 katika kikao kazi cha viongozi hao wa michezo wa kitaifa kilichofanyika katika Ukumbi wa Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es salaam.
Amesema kuwa mambo mengine muhimu ni kukuza na kuendeleza mchezo husika kwa ujumla wake na kuboresha viwango vya wachezaji na uchezaji wao pamoja na ufundishaji wa mchezo.
Aidha, amesisitiza pia, uamuzi katika michezo, uongozi na utawala wa vyama, mashirikisho pamoja na kamati za michezo sambamba na tiba ya wanamichezo ni masuala ya kuzingatiwa katika kuhakikisha michezo inaendelea.
"Kazi kubwa ya Chama cha mchezo kitaifa ni kusimamia maendeleo ya mchezo huo na kuwaunganisha wanamichezo," amesema Neema.
Aidha ameendelea kusema kutoa huduma kwa wachezaji, walimu na wanachama wake katika Mafunzo, kutekeleza kwa ukamilifu maelekezo yanayotolewa na vyombo vya juu vya michezo ikiwamo kuwasilisha kwa BMT ni muhimu kuzingatiwa na viongozi wa michezo.
Ameongeza kuwa viongozi wa hao wanatakiwa kuwasilisha kalenda za Kila mwaka, mpango mkakati wa Chama wa muda mrefu na mfupi, kuwasilisha anuani za ofisi pamoja na mitandao ya kijamii.
Amesema kuwa wanatakiwa kuwasilisha mahesabu ya kila mwaka, kulipa ada ya BMT ya kila mwaka na kupata idhini ya BMT katika mashindano yote ya kitaifa na kimataifa yanaratibiwa na wadau hao.