MSITHA ATOA KONGOLE KWA MAJESHI
service image
20 Sep, 2022

Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Neema Msitha amelipongeza Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMATA) kupitia programu yao na Shirikisho la Kimataifa CISM katika kuendeleza michezo nchini.

Pongezi hizo amezitoa leo Septemba 20, 2022 alipoalikwa katika ufunguzi wa mafunzo ya ukocha wa mpira wa Wavu na kikapu uliofanyika jijini Dar Es Salaam.

Neema amesema anayapongeza Majeshi yote kwa mchango mkubwa katika maendeleo ya michezo.

"Tumeshuhudia kupitia Baraza lao wametengeneza Urafiki na Ujerumani kwa kutoa mafunzo kwa makocha na imani kubwa ushirikiano huu utasaidia michezo kupiga hatua," amesema Neema.

Amesema BMT itaendelea kuwaunga mkono na milango ipo wazi katika kushirikiana na wanaendelea na vikao na BAMATA kuweka mipango ya pamoja kuendeleza michezo nchini.

Neema ametoa rai kwa vyama vya michezo nchini kuiga mfano wanapopata fursa kama hiyo ya kutengeneza Urafiki kwa waliopiga hatua katika michezo kwa kuwezesha kupata vifaa vya michezo na wataalam.

Kwa upande wake Mgeni rasmi, Brigedia Jenerali Selemani Gwaya, alisema lengo la mafunzo hayo ni kuboresha ushiriki wamataifa wanachama katika CISM, kupata wakufunzi wenye sifa stahiki kutoka kwa marafiki hao.

Aliongeza kuwa, ni pamoja na kujenga mshikamano wa CISM na usaidizi wa kiufundi kwa kutoa mafunzo, vifaa vya michezo, Kambi za mafunzo kwa wanamichezo, kozi au semina kwa Makocha na wakufunzi na kuhudhuria mashindamo ya CISM.

"Nitoe rai kwa wanafunzi kuhudhuria kwa dhati mafunzo haya mkubwa na lengo la kuongezea weledi na maarifa Ili mchangie mafanikio ya timu zenu na maendeleo ya michezo Majeshi na nchi kwa ujumla,"alisema Brigedia Jenerali Gwaya.

Zaidi ya washiriki 100 kutoka majeshi mbalimbali wanatarajia kunufaika na mafunzo ya ukocha wa mpira wa kikapu na Wavu yaliyofunguliwa leo Septemba 20 na yatahitimishwa Septemba 29 Jijini Dar es Salaam.