BMT WAIWEZESHA TIMU YA TAIFA YA NGUMI “FARU WEUSI”
Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limeiwezesha Timu ya Taifa ya Ngumi “Faru Weusi” kwa kugharamia posho, malazi na chakula, kama sehemu ya maandalizi ya kuongeza ushindani katika Mashindano ya IBA Ubingwa wa Dunia.
Mashindano hayo yanaanza leo, Desemba 4, 2025, jijini Dubai, U.A.E., ambapo bondia wa Timu ya Taifa, Enzi Kasililika, atafungua kampeni ya Tanzania kwa kupanda ulingoni dhidi ya Joshua Cousin wa Seychelles.
Kasililika atashindana katika uzani wa kilo 75 (Middleweight), kwenye bout ya 37 ya Session 2, inayotarajiwa kuanza saa 2:00 usiku katika Uwanja wa Tennis wa Dubai Duty Free. Mashindano haya yanashirikisha mataifa 108 na yanahusisha uzani 13 kwa upande wa wanaume.
Tanzania “Faru Weusi” inawakilishwa na mabondia watano ambao ni Enzi Kasililika wa uzani wa kilo 75 (Middleweight), Rashidi Mrema wa uzani wa kilo 60 (Lightweight), Faki Faki wa uzani wa kilo 54 (Bantamweight), Juma Athumani wa uzani wa kilo 51 (Flyweight) na Ally Ngwando wa uzani wa kilo 48 (Minimumweight),
Wachezaji hao wanaongozwa na Mwalimu Mkuu Samwel Kapungu ‘Batman’.

