BARAZA LA MICHEZO LA TAIFA (BMT), LIMETAKIWA KUENDESHA PROGRAMU MAALUM AMBAYO ITALENGA KUONGEZA USHIRIKI WA WANAWAKE KATIKA MCHEZO WA KARATE NCHINI.

Baraza la Michezo la Taifa (BMT), limetakiwa kuendesha programu maalum ambayo italenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika mchezo wa karate nchini.
Agizo hilo limetolewa leo tarehe 9 Oktoba, 2022 na Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Saidi Yakubu alipokuwa anafunga mafunzo ya mchezo wa Karate yaliyofanyika nchini kwa takribani siku 6 katika ukumbi wa Starlite Masaki jijini Dar es Salaam, ambapo amesema mchezo huo ni miongoni wa michezo inayofanya vizuri katika medani ya kimataifa hivyo ni vyema BMT kwa kushirikiana na Chama kuhakikisha wadau wengi zaidi wanajitokeza kucheza Karate kwa ajili ya afya na kujilinda.
“serikali sasa itatilia mkazo ushiriki wa wanawake katika mchezo wa karate,Tanzania kuna takribani watu milioni mbili ambao wajihusisha na mchezo huu katika mikoa mbalimbali hapa nchini,na katika hao wanawake hawazidi elfu moja, na ndio maana nimetoa maagizo kwa BMT kuendesha programu maalum ambayo itaongeza ushiriki wa wanawake katika mchezo wa karate,”alisema Yakubu.
Aidha amekipongeza Chama cha mchezo wa karate nchini (TASHOKA) kwa kufuta ada za wanawake katika ‘dojo’ mbalimbali nchini, lengo likiwa ni kutoa hamasa kwa wanawake pamoja na watu wenye mahitaji maalum kuongezeka katika mchezo wa karate.
“nawapongeza sana viongozi wa TASHOKA kwa upande wao kuona umuhimu wa kufuta ada za wanawake katika ‘madojo’ hapa nchini, ili nao waweze kuhamasika na kushiriki kwa wingi katika mchezo huu,”alisema Yakubu.