BMT NA MRADI WA KIMKAKATI

Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kupitia kwa Mtendaji wake Mkuu Bi. Neema Msitha leo tarehe 13 Januari, 2025 limeingia mkataba rasmi na kampuni ya Volumetric Arch Consult Limited kwa ajili ya kutoa huduma za ushauri elekezi kwa mradi wa ujenzi wa Kituo cha Mafunzo ya Michezo ya Viwango vya Juu (High-Performance Sports Training Centre) uliopo Mkoani Manyara.
Mkataba huu, wenye namba TR17/2024/2025/C/07, unajumuisha utafiti wa uwezekano wa mradi (Feasibility Study), tathmini ya athari za mazingira na kijamii (ESIA), ubunifu wa kina wa mradi (Detailed Designing), kuandaa makadirio ya gharama (BOQ), kuandaa nyaraka za zabuni (Tender Documents) na usimamizi wa ujenzi wa kituo hicho.
Mradi huu unalenga kuboresha maendeleo ya michezo nchini kwa viwango vya kimataifa kwa kuhakikisha wanamichezo wanapata mazingira bora ya mafunzo na maandalizi. Baraza linaendelea kushirikiana na wadau wote wa michezo ili kufikia malengo makubwa ya mafanikio ya michezo nchini.