BMT YATETA NA WASIMAMIZI WA MICHEZO MKOA WA DAR ES SALAAM
service image
04 Mar, 2025

Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kupitia Kitengo cha Usajili leo tarehe 4 Machi 2025 kimefanya kikao na Maafisa Michezo wa Mkoa wa Dar es Salaam kuweka sawa usimamizi wa sekta ya hiyo Mkoani hapo.Kikao hicho kililenga kubadilishana taarifa na kuweka mikakati thabiti ya kusimamia maendeleo ya michezo katika ngazi ya mkoa na wilaya za Mkoa huo.

Kaimu Msajili wa Vyama vya Michezo Tanzania Wakili Abel Ngilangwa ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa kikao hicho amesisitiza umuhimu wa kushirikiana ili kuhakikisha kuwa michezo inasimamiwa kwa mujibu wa sheria na kanuni.

Aliongeza kuwa, Kitengo cha Usajili dhamira yake ni kuhakikisha vyama, vilabu, na waandaaji wa mashindano wanasajiliwa kwa mujibu wa sheria, huku akisisitiza usimamizi wa 'gym' nao unapaswa kuimarishwa ili kutoa mchango stahiki katika maendeleo ya michezo.

Hata hivyo Baraza limepokea taarifa kuhusu hali ya michezo katika Mkoa wa Dar es Salaam na kuweka mpango wa kuhakiki 'gym' zote zilizopo zinasimamiwa kwa kufuata miongozo iliyopo.

Ngilangwa, amesisitiza mambo matatu muhimu kwa maendeleo ya michezo nchini ikiwemo, ligi zote kuhusisha vilabu vilivyosajiliwa, waandaaji wa matukio ya michezo lazima wawe wamesajiliwa, na ushirikiano kati ya BMT, Ofisi za Maofisa Michezo wa Mikoa na wilaya ni muhimu katika kuhakikisha usimamizi thabiti wa michezo.

BMT itaendelea kushirikiana na wadau wote ili kuhakikisha michezo inakuwa na kuleta maendeleo kwa Taifa.