BMT YAGHARAMIA WACHEZAJI 20 MASHINDANO YA DUNIA

Baraza la Michezo la Taifa 'BMT,' limegharamia jumla ya wachezaji 20, ambao watano (5) ni mabondia wakike wa Timu za Taifa ya Ngumi za Ridhaa na 15 wa Mchezo wa Kabadi kwa ajili ya kuiwakilisha Tanzania katika michuano ya Dunia.
Hayo yamejiri leo Ijumaa, Februari 28, 2025 kwa nyakati tofauti katika kikao cha Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa BMT Bi.Neema Msitha na viongozi wa Chama cha Ngumi za Ridhaa 'BFT' na wa mchezo wa Kabadi kwa ajili ya kujadili maandalizi ya Timu hizo zinatarajia kwenda nchini Serbia na Uingereza kushiriki mashindano hayo.
Wachezaji watano wa kike wa Timu ya Taifa ya Ngumi za Ridhaa wanatarajia kwenda kuiwakilisha nchi katika mashindano ubingwa wa Dunia wanawake yanayotarajia kutimua vumbi kuanzia Machi 3 hadi 17, mwaka huu katika mji wa Nis nchini Serbia wakati timu ya Taifa ya mchezo wa Kabadi jumla wa wachezaji 15 wataiwakilisha nchi katika mashindano ya Kombe la Dunia ambayo yanatarajiwa kuanza Machi 15, mwaka huu kwenye mji wa Birmingham, Uingereza.
Kwa upande mwingine, Bi Msitha amewataka viongozi wa vyama vyote vya michezo vya taifa kuusoma mwongozo wa Serikali wa kuzisaidia timu za taifa, nakusema kuwa Serikali kupitia BMT itazisaidia timu kwa asilimia 25 tu pale inapowezekana huku vyama vyenyewe vikitakiwa kuchangia kwa asilimia 75, hivyo viache kuitegemea serikali peke yake.