BMT YAKUTANA NA KAJUMULO WORLD SPORTS KUKUZA NA KUTAMBULISHA MICHEZO MIPYA TANZANIA
Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limefanya kikao na Mkurugenzi wa Kampuni ya Kajumulo World Sports, Bw. Charles Sixbert, kutoka nchini Marekani, kujadili uwekezaji katika sekta ya michezo nchini, hususan kutambulisha michezo mbalimbali ambayo bado haijaanza kuchezwa Tanzania.
Kikao hicho kimefanyika leo Januari 14, 2026, kikilenga kujadili mikakati ya kuitangaza na kuitambulisha michezo hiyo nchini Tanzania, pamoja na fursa za kuipeleka michezo hiyo kuchezwa katika nchi za Canada na Marekani.
Aidha, kikao hicho kimejadili namna ya kubaini na kukuza fursa zitokanazo na michezo, ikiwemo upatikanaji wa ajira kwa vijana, pamoja na kuwajengea uwezo walimu na wataalamu wa michezo kupitia mafunzo ya ndani na nje ya nchi.
Ujumbe wa BMT uliwakilishwa na Afisa Michezo Mwandamizi, Bw. Charles Maguzu, huku Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ikiwakilishwa na Bw. Mlinde Mahona.
Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Maguzu amesema BMT iko tayari kushirikiana na wadau wa michezo wa ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha sekta ya michezo inaendelea kukua, kuimarika na kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini Tanzania.

