BMT YATOA MSAADA KWA SOCCER ACADEMY (CHANIKA)
service image
11 Jan, 2026

Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limefanya ziara na kutoa msaada wa mipira mitano kwa Kituo cha Mafunzo ya Mpira wa Miguu cha 'Kibadeni International Soccer Academy' kilichopo Zogoali, Chanika, Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam, Januari 9, 2026.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo, Afisa Michezo Mwandamizi wa BMT, Charles Maguzu, alimpongeza Mzee Kibadeni kwa kuanzisha kituo hicho chenye lengo la kukuza vipaji vya soka kwa vijana. Aliwahimiza vijana waliopo kituoni hapo kutumia kikamilifu fursa waliyoipata kwa kujituma, kufanya mazoezi kwa bidii na kuendeleza vipaji vyao ili kujipatia ajira, kuchezea vilabu vikubwa na hatimaye kuwa tunu ya kuitumikia Timu ya Taifa.

Maguzu pia aliwasisitiza vijana hao kuzingatia nidhamu, upendo na mshikamano, akibainisha kuwa misingi hiyo ni muhimu katika kufanikisha malengo yao na kuona matokeo chanya ndani ya miaka michache ijayo.

Kwa upande wake, mmiliki wa kituo hicho, Abdallah Kibadeni Mputa, aliishukuru BMT kwa msaada huo, akisema utawajengea ari na kuongeza ufanisi kwa vijana wanaokuzwa kisoka katika kituo chake.

Aidha, katika ziara hiyo, BMT waliambatana na viongozi wa Umoja wa Maveterani wa Soka Tanzania (UMUSOTA), ambao nao walikabidhi seti moja ya jezi kwa kituo hicho, ikiwa ni mchango wa kuimarisha mazingira ya mafunzo na kuendeleza vipaji vya vijana.