BMT YAWATAKA 'FEAUS' KUYATEKELEZA MAAZIMIO YA KAMBI KWA VITENDO

Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limewataka Viongozi wa Shirikisho la Michezo ya Vyuo Vikuu Afrika Mashariki "FEAUS" kuyatekeleza maazimio ya kambi yao ili kufikia lengo ikiwemo kuzingatia utawala bora katika michezo namna kuandaa matukio ya michezo, uwezo wa kujiamini katika uongozi na kuratibu maswala mbalimbali yahusuyo michezo vyuoni.
Hayo yameelezwa leo Oktoba 09, 2022 na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Michezo BMT Halima Bushiri kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wakati akifunga kambi ya siku mbili iliyowakutanisha katika Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima "Institute Adult Education-IAE" Morogoro tarehe 8 na 9 Octoba 2022.
Halima amewapongeza viongozi hao kukutana na kuyajenga kwa pamoja masuala mbalimbali yahusuyo maendeleo ya michezo katika Vyuo Vikuu vya nchi za Afrika Mashariki.
"Nawapongeza sana kwa kambi hii, nendeni kayatekelezeni kwa vitendo maazimio ya kambi yenu,"alisisitiza Halima.
Kambi hiyo imewakutanisha viongozi 79 kutoka vyuo 18, vikiwemo 7 kutoka Kenya, 10 kutoka Tanzania na kimoja (1) kutoka Uganda, pamoja na viongozi 79.