Dkt. Abbasi:Ni hamasa kwa Tanzania kufika kombe la dunia

Na. Najaha Bakari - DSM
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi katika hafla ya kupokea kombe halisi ya Dunia (Fifa World cup Trophy Tour) linalotarajia kufika nchini siku ya jumanne Mei 31, 2022.
Kombe hilo linaletwa na Kampuni ya kinywaji cha Coca Cola ambapo pia inamleta aliyewahi kuwa nguli wa Barcelona FC na Chelsea, Juliano Belletti.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mkutano nao leo Mei 28,2022 Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi alisema kombe hilo litawasili nchini siku ya Jumanne na Rais Samia atakuwa mgeni rasmi katika hafla ya kupokea kombe hilo la Dunia la Fifa la mchezo wa Soka.
Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi nne ikiwemo Kenya, Ethiopia na Afrika Kusini ambazo zimepata nafasi ya kutembelewa na kombe hilo ambalo ni hamasa kubwa kwa Taifa kupigania kufanikiwa kutafuta nafasi ya kucheza kombe la Dunia.
“Ujio wa kombe hilo ni hamasa kwa Tanzania kuhakikisha tunakuwa tayari kwa timu yetu ya soka (Taifa Stars) tunaenda kushiriki michuano hiyo na ikiwezekana kombe hili liweze kubaki,” alisema Katibu huyo.
Alisema katika hafla hiyo Rais Samia Suluhu Hassan ataungana na baadhi ya wawakilishi na wadau wa michezo kutoka nasaha zake katika sekta ya michezo.
Katibu huyo alisema baada ya hafla hiyo Juni Mosi, mwaka huu litapelekwa uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya kutoa fursa Watanzania na wananchi kupiga picha na kombe hilo.
Naye Mkurugenzi wa masoko wa Kapuni ya Coca Cola, Josephine Msalilwa alisema juni Mosi mwaka huu itakuwa siku ya Watanzania kupiga picha na atakuwepo na mchezaji nguli aliyewahi kucheza kombe la Dunia, Belletti.
“Mbali na kupiga picha lakini pia katika ziara ya kombe la Dunia kutakuwa na burudani mbalimbali kwa ajili ya Watanzania ambao watakuja kupiga picha ikiwa ni kumbukumbu zao katika maisha,” alisema Josephine.