DOKTA ABBASI AWATAKA VIONGOZI WA CHANETA KUREJESHA MCHEZO HUO KATIKA RAMANI YA KIMATAIFA
service image
25 May, 2022

Katibu Mkuu wa wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dokta Hassan Abbasi amewataka viongozi wa Chama cha mchezo wa Netiboli Tanzania (CHANETA) kuja na mipango mikakati mikubwa itakayoweza kurejesha mchezo huo katika ramani ya michezo Bora kwa kufanya vizuri kitaifa na kimataifa.

Dkt. Abbasi ametoa agizo hilo leo tarehe 25 Mei, 2022 alipokutana na kufanya kikao na viongozi wa Chama hicho katika moja ya kumbi za uwanja wa Benjamini Mkapa Jijini Dar es Salaam ambapo amesema Netiboli ni moja michezo ya kipaumbele hivyo ni vyema viongozi wakatumia fursa waliyopata kuendelea kuutangaza mchezo huo kwa kuandaa mashindano mbalimbali ambayo yatawavutia wadhamini kujitokeza na kurejesha hadhi ya mchezo wa Netiboli nchini.

“niwapongeze sana viongozi wapya mlioingia kukiongozi Chama cha Netiboli,lakini mna kazi kubwa sana ya kuhakikisha mchezo unarejea katika hadhi yake ya awali hususani kimataifa,nilishakutana na viongozi waliokuwepo na kutoa maagizo,tuondoe doa lililowekwa la kutokushiriki mashindano ya kimataifa,lakini mnapaswa kuja na mipango mikakati mikubwa ambayo itaendeleza mchezo huu hapa nchini,”alisema Dkt. Abbasi

Aidha Dkt. Abbasi amewahakikishia viongozi wa CHANETA kuwa Serikali itakuwa nao bega kwa bega katika harakati zote kwa kuinua zaidi mchezo huo, na kuwataka kuishirikisha BMT katika kila hatua ya maendeleo ya mchezo ikiwemo na mkakati wa kuboresha viwanja vya mchezo wa Netiboli nchini.

“kama mchezo moja wapo wa kipaumbele hapa nchini, niwahakikishie kuwa Serikali itakuwa nanyi bega kwa bega kuinua mchezo huu, muwe mnaishirikisha BMT katika mikakati yenu ya kimaendeleo, ni vyema mkaja na mikakati mikubwa kama vile kuboresha viwanja vya mchezo wa Netiboli pamoja na mapendekezo ya kujenga viwanja vingine katika kila mkoa,”alisema Dkt. Abbasi.