JATA YAPATA VIONGOZI WAPYA
Chama cha Mchezo wa Judo Tanzania (JATA) kimefanya uchaguzi leo, Januari 17, 2026, na kupata viongozi wapya watakaokiongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka minne. Uchaguzi huo umefanyika katika ukumbi wa Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Katika uchaguzi huo, Richard Marton Ndayirukiye amechaguliwa kuwa Rais wa JATA, huku nafasi ya Makamu wa Rais ikichukuliwa na Andrew Thomas Mlugu.
Kwa nafasi ya Katibu Mkuu, amechaguliwa Yohana Edward Jiji, wakati Katibu Mkuu Msaidizi akichaguliwa Saleh Baraka Saleh. Nafasi ya Mweka Hazina imechukuliwa na Lawrence Peter Maganga.
Aidha, Michael Jeremia Kweka amechaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Waamuzi, huku Clement Lubasha Mabala akichaguliwa kushika nafasi ya Mkurugenzi wa Ufundi. Nafasi ya Mkurugenzi wa Ustawi, Elimu na Kujitolea imechukuliwa na Raphael Daud Raphael.
Uongozi mpya wa JATA unatarajiwa kuimarisha maendeleo ya mchezo wa judo nchini, kukuza vipaji, kuboresha mifumo ya mashindano na kuipeleka Tanzania katika viwango vya juu vya kimataifa.

