KIKAO NA VIONGOZI WA RIADHA.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Bi. Neema Msitha leo Tarehe 29 Aprili, 2024 amefanya mazungumzo na Viongozi wa Shirikisho la Riadha Tanzania (AT) na kutoa maelekezo kadhaa yanayotakiwa kutekelezwa mapema ili kurudisha hadhi ya mchezo huo nchini.
Msitha amewataka Viongozi hao kufanya vikao vya kikatiba na wanachama wao kujibu hoja na maswali ili kuondoa changamoto mbalimbali katika chama.
Pia wameelekezwa kukutana na wadau wanaoandaa mbio za barabarani ili kusikiliza hoja zao na kufanya maboresho yanayostahili.
"Wekeni mpango wa kutoa taarifa kwa wadau kupitia vyombo vya habari ili kuendelea kuweka imani ya chama kwa wadau wenu,"alisema Msitha.
Vilevile amewataka Viongozi hao kuwasilisha taarifa ya mbalimbali kwa mujibu wa taratibu ikiwemo taarifa ya fedha BMT kabla ya tarehe 03 Mei, 2024.
Kwa upande wake Rais wa Shirikisho hilo Silas Isangi amemshukuru Mtendaji Mkuu wa Baraza kwa kikao hicho na kuahidi kutekeleza maagizo yake kwa wakati.
Kikao hicho kilimhusisha Bi. Neema Msitha Katibu Mtendaji wa Baraza, Rais wa AT Silas Msangi na Makamu wake William Kalaghe na Maafisa wengine wa Baraza.