TIMU YA TAIFA YA TANZANIA YA RIADHA KWENDA MAREKANI KWENYE MAANDALIZI
service image
06 Jan, 2026

Timu ya Taifa ya Tanzania ya mchezo wa riadha imeondoka leo Januari 6 2026 kuelekea nchini Marekani kwa ajili ya maandalizi ya Mashindano ya Mbio za Nyika yatakayoanza Januari 10 mwaka huu.

Wanariadha waliokwenda ni Sinda Daniel, Ambrose Sadikiel, Elizabeth Boniphace na Regina Deogratius ‘Mixed Relay 2 km ‘, pamoja na Gabriel Geay, Emanuel Dinday, Benjamin Raysim, John Welle na Inyasi Sulley ‘Senior Men 10 km’.

Akizungumza wakati wa kukabidhi Bendera ya Taifa na kuiaga timu hiyo, Ofisa Michezo Mwandamizi wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Bw. Charles Maguzu, aliwataka kwenda kuonyesha uzalendo, ushirikiano Aidha, amewahakikishia wachezaji wote kuwa BMT itaendelea kushirikiano nao hata watakapokuwa nje ya nchi na kuilinda heshima ya Tanzania kwa kupigania medali.

“Nendeni mkaonyeshe uzalendo na kulinda heshima ya nchi kupitia mashindano haya ambayo ninaamini yatakuwa na upinzani mkubwa,” alisema Maguzu, akiongeza kuwa maandalizi ya muda mrefu waliyoyafanya yanawapa nafasi kubwa ya kufanya vizuri.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Bw. Stephen Rogath, alisema ana imani kubwa na kikosi hicho kutokana na mazoezi na maandalizi waliyoyafanya.

Nahodha wa timu, Gabriel Geay, alisema wanariadha wamejipanga kikamilifu kupata ushindi.

“Malengo yetu ni kupata ushindi katika mashindano haya, tunaomba Watanzania waendelee kutuombea ili tupate medali za dhahabu,” alisema Geay.