MHE.MCHENGERWA: TUHAKIKISHE VILABU VYOTE NCHINI VINAENDESHWA KISAYANSI NA KUWA NA TIMU ZA VIJANA
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa (Mb) amewataka watendaji wake katika tasnia ya michezo,kuhakikisha kuwa vilabu vyote vya michezo nchini vinaendeshwa kisayansi sambamba na kuwa na timu za vijana kwa ajili ya kuendelea kupiga hatua zaidi michezoni.
Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo leo tarehe 19 Aprili, 2022 katika moja ya kumbi za shule ya Sekondari Azania mara baada ya kuzindua Maabara ya Kompyuta iliyojengwa kwa udhamini wa mchezo wa Baseball kupitia kwa familia ya Robinson na klabu ya mchezo wa Baseball ya Los Angeles Dodgers kutoka Marekani, ambapo pia amewataka viongozi wa chama cha mchezo wa Baseball (TaBSA) kufuatilia kwa karibu utunzaji na utumiaji wa vifaa vilivyotolewa.
“wizara yangu yenye dhamana ya michezo tujipange katika kuweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha vilabu vyote vya michezo nchini vinaendeshwa kisayansi na vinakuwa na timu za vijana,nadhani wakurugenzi mmenisikia vizuri,lakini pia nyinyi viongozi wa TaBSA msimamie kwa ukaribu vifaa vinavyoletwa na wafadhili kwani kwa kufanya hivyo wataendelea kupata imani na kuleta ufadhili mwingine zaidi na zaidi,”alisema Mhe. Mchengerwa.
Aidha Mhe. Mchengerwa amezitaka Halmashauri nchini kuendelea kutenga Bajeti ya kutosha kwa ajili ya kugharamia michezo hasa kwa vijana sanjari na kutumia fursa hiyo kutengeneza timu zitakazoweza kutoa ushindani katika mashindano mbalimbali.
“lakini sita Mheshimiwa Waziri Mkuu katika hotuba yake angependa kuona Halmashauri zinaendelea kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya kugharamia michezo hasa kwa vijana sanjari na kutumia fursa hiyo kutengeneza timu zitakazoweza kutoa ushindani katika mashindano mbalimbali,”alisema Mhe. Mchengerwa.