MHE.MHAGAMA AMEWAGIZA WAAJIRI WOTE NCHINI KUHAKIKISHA WANAMICHEZO WANASHIRIKI MICHEZO YA SHIRIKISHO LA MICHEZO YA WIZARA,IDARA ZA SERIKALI NA MIKOA (SHIMIWI)

Waziri wa Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amewagiza waajiri wote nchini kuhakikisha wanamichezo wanawezeshwa kushiriki michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara,Idara za Serikali na Mikoa (SHIMIWI), huku akitaka wanamichezo kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za michezo pamoja na Utumishi wa Umma.
Mhe. Mhagama ametoa agizo hilo leo Oktoba 05, 2022, wakati akifungua michezo ya SHIMIWI katika uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga, ambapo amesema michezo hiyo ni moja ya njia ya kuimarisha mahusiano mazuri ya kikazi baina ya wafanyakazi wa wizara mbalimbali pamoja na Taasisi za kiserikali.
"Nitumie nafasi hii kuwahamasisha Watumishi wa Umma kushiriki mashindano haya kwa wingi, lakini hawawezi kushiriki bila waajiri wao kuhakikisha wanamichezo wanawezeshwa vyema kushiriki michezo hii, kwani tunaelewa kuwa kupitia michezo hii licha ya kujenga afya zetu, lakini pia njia moja wapo ya kuimarisha mahusiano mazuri ya kikazi baina yetu,”alisema Mhe. Muhagama.
Aidha Mhe. Jenista Muhagama amewagiza waandaaji wa Mashindano ya SHIMIWI kuhakikisha watumishi wenye ulemavu wanashiriki kikamilifu mashindano hayo.
Jumla ya Timu 63 kutoka wizara 27, Mikoa 18, Idara za Serikali 18 zinashiriki michezo hiyo iliyobeba Kauli mbiu "Michezo hupunguza magonjwa yasiyo ambukiza na kuongeza tija mahala pa kazi, Kazi Iendelee"