BMT NA JICA WAFANYA MAFUNZO YA UTIMAMU WA MWILI KWA MAVETERANI WA SOKA
Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Japani (JICA), Leo tarehe 9 Oktoba, 2025 wameendesha mafunzo maalum ya utimamu wa mwili kwa wanachama wa Umoja wa Maveterani wa Soka Tanzania (UMSOTA) katika makao makuu ya umoja huo yaliyopo Magomeni, jijini Dar es Salaam.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uelewa washiriki kuhusu umuhimu wa mazoezi ya mwili kwa afya na ustawi wa wachezaji wastaafu, pamoja na namna bora ya kudumisha utimamu wa mwili hata baada ya kustaafu michezo ya ushindani.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Bw. Charles Maguzu Afisa Michezo wa Baraza na moja ya wakufunzi wa mafunzo hayo, alieleza kuwa, BMT itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo JICA kuhakikisha michezo inakuwa sehemu ya maisha ya Watanzania wote bila kujali umri wao.
Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za serikali kupitia BMT katika kuhamasisha mazoezi ya mwili kwa makundi yote ya jamii ili kujenga taifa lenye afya bora na lenye tija.

