KUAHIRISHWA CHAN KUMETUPA NAFUU
service image
15 Jan, 2025

Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Leodger Tenga amesema Kuahirishwa kwa fainali za mataifa kwa wachezaji wa ndani 'Chan' kumewapa nafuu kubwa ya kuendelea na maandalizi.

Michuano ya Chan ilitarajiwa kufanyika kuanzia February mosi mwaka huu nchini Tanzania, Kenya na Uganda lakini Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF) lilitoa taarifa ya kuahirisha jana hadi Agosti mwaka huu.

Akizungumza kwenye kongamano la wadau wa michezo kuelekea fainali za Chan 2024 na Afcon 2027, Tenga amesema miezi mitatu waliyopewa kuandaa michuano hiyo ilikuwa michache lakini walifurahi licha ya kuwa walijua ni mzigo mkubwa.

Amesema katika miaka yake 40 ya kuwa kwenye michezo hajawahi kuona nchi inapewa miezi mitatu kuandaa mashindano makubwa kama hayo ila waliendelea na maandalizi na serikali ilikuwa mstari wa mbele kufanikisha.

"Kuahirisha kwa mashindano nchi imepata ahueni kubwa sana ingawaje sisi tulikuwa tayari Uwanja wa Benjamin Mkapa na Amaan Zanzibar vipo katika hali nzuri sana, Viwanja vya mazoezi vipo pia, katika hali nzuri kwa hiyo jambo la kuongeza muda limetupa muda zaidi tuwe wenyeji wazuri zaidi,"amesema.

Amesema zipo fursa za kiuchumi na kijamii hivyo ni wajibu wa kizitumia ipasavyo.