MSAJILI AWATAKA AT KUZINGATIA SHERIA, DEMOKRASIA NA UTAWALA BORA KATIKA KUSIMAMIA RIADHA TANZANIA

Kaimu Msajili wa Vyama vya Michezo nchini Wakili Evordy Eliezer Kyando amewataka Viongozi wa Shirikisho la Riadha Tanzania (AT) kuzingatia matakwa ya Sheria na taratibu mbalimbali katika kufanya shughuli za mchezo huo nchini.
Rai hiyo ameitoa leo tarehe 6 Oktoba, 2023 katika ofisi yake iliyopo katika Uwanja wa Benjamin akiwa katika kikao na Katibu wa Shirikisho hilo Jackson Ndaweka kujadiliana mambo kadhaa ya kulijenga shirikisho hilo.
Msajili Kyando amehimiza Shirikisho hilo pamoja na vyama shiriki vilivyo chini yake kuhakikisha wadau wake wanaofanya michezo chini yao wanasajili asasi zao ipasavyo sambamba na kulipa ada za mwaka kabla ya kuruhusiwa kuendesha shughuli wanazoomba kuzifanya.
"Wajibu wa shirikisho lako ni kuhakikisha sekta hii inakuwa tulivu na yenye amani wakati wote,"alisema Kyando.
Aliendelea kwa kuwataka kusimamia ipasavyo utoaji wa vibali vya matukio ya michezo ya mbio maarufu kama "Marathon" ili kubaini wote wanaoendesha matukio bayo pasipo kusajiliwa na ofisi yake huku akisisitiza
umuhimu wa kuzingatia misingi ya utawala bora na demokrasia kwa kuhakikisha wanachama na Umma wanapata taarifa juu ya masuala mbalimbali yanayoendelea katika Shirikisho.
Kwa upande wake, Katibu huyo wa AT Wakili Jackson Ndaweka amemhakikishia Msajili kuzingatia maelekezo ya Serikali na kuwa atatumia nafasi yake kuelimisha wadau wanaofanya shughuli zao chini ya AT ili watii Sheria pasipo shuruti na kudumisha Demokrasia na Utawala Bora katika Shirikisho.
Msajili katika kikao hicho aliambatana na Mkaguzi wa ndani George Otieno na Afisa Michezo anayesimamia riadha.