SAMIA WOMEN BOXING CHAMPIONSHIP 2025
service image
28 Jan, 2025

Mashindano mapya ya ngumi ya Wanawake ya Samia "SAMIA WOMEN BOXING CHAMPIONSHIP 2025" yanatarajiwa kauanza Ijumaa 31 Januari, 2025 mpaka 2 Februari, 2025 katika fukwe za Kawe Beach Club, Dar es salaam.

Mashindano hayo yaliyoasisiwa na Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT) yanalenga kuongeza hamasa kwa Wanawake katika mchezo wa ngumi nchini na yatatumika kuchagua wachezaji watakao jiunga na kikosi cha Timu ya Taifa kujiandaa kushiriki kwa mara ya pili katika mashindano ya 14 ya Ubingwa wa Dunia yatakayofanyika Nis, Serbia kuanzia tarehe 6-17 machi, 2025.

"Hii itakua ni mara ya pili kwa Taifa kushiriki mashindano ya Ubingwa wa Dunia, baada ya kufanya hivyo kwa mara ya kwanza kwanye mashindano ya 13 yalifanyika New Delhi, India mwezi wa tatu, 2023...Maandalizi ya mashindano yetu yanaendelea vizuri, tunawaomba wadau mjitokeze kwa wingi kutuunga mkono kwa hali na mali" Alinukuliwa Asha George Voniatis, Mwenyekiti wa kamati ya wanawake na wachezaji ya BFT na mjumbe wa kamati ya usawa kijinsia ya Afrika (AFBC).

Mashindano haya yatashirikisha wachezaji wanawake wanaocheza ngumi za ridhaa na za kulipwa kupitia kamisheni ya ngumi za kulipwa (TPBRC).

Pamoja na mashindano hayo, wachezaji wote watahudhuria semina za kuwawezesha, kuwajengea maarifa ya maisha na Ujasiliamali kwa kushirikina na taasisi ya ARHN ya Mbezi Beach, Dar es salaam.

Wachezaji wote Wanawake nchini Tanzania mnaombwa mjitokeze kwa wingi kushiriki mafunzo na mashindano haya.