SERIKALI YATUNISHA MIFUKO YA GEAY NA SIMBU
service image
27 Apr, 2023

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Dkt. Pindi Chana kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) amewakabidhi Gabriel Geay kitita cha shilingi milioni tatu (3) na Alphonce Simbu shilingi milioni mbili (2) kwa kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania pamoja na kutoa hamasa kwa wanamichezo wengine kujituma zaidi.

Hayo yamefanyika leo Aprili 27, 2023 kuwapongeza wanariadha hao, Gabriel Geay aliyeibuka mshindi wa pili (2) mbio za Boston Marathon, 2023 nchini Marekani na Alphonce Simbu aliyeibuka na ushindi wa tatu (3) katika mbio za nchini China, tukio hi Bungeni Jijini Dodoma.

"Tunahitaji vipaji vingi kwa vijana katika michezo yote na Serikali ipo tayari kuviendeleza katika shule 56 zilizotengwa, nanyi tunaomba muendelee kuwa mfano wa vijana wengine na Serikali iko pamoja nanyi "alisema na kuongeza kuwa;

"Tutaendelea kutoa mafunzo na semina kwa wanamichezo na wataalam ili taifa liweze kuwa na viwango vya kimataifa vingi katika michezo yote ili kuliwakilisha vyema katika mashindano ya kimataifa,"alisisitiza.

Aidha, Waziri Pindi Chana amewataka wadau mbalimbali kushirikiana na Serikali kulisukuma gurudumu la maendeleo ya michezo nchini, ikiwemo kujenga miundombinu sambamba na kuwasaidia wanamichezo kufikia ndoto zao.

Awali Naibu Waziri Hamis Mwinjuma ameeleza kuwa, Serikali kuanzia sasa inaanza maandalizi ya michezo ya Olimpiki Paris nchini Ufaransa 2024.