SILAS AWAPONGEZA WANARIADHA KWA KIWANGO WALICHOONYESHA

Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (AT) Silas Isangi amewapongeza wanariadha kwa kiwango walichoonyesha ingawa maandalizi hayakuwa ya muda mrefu katika mashindano ya Afrika Mashariki ya vijana wa umri wa chini ya miaka 18 na 20 yaliyofanyika kwa siku mbili (2) kuanzia Mei 27 na kuhitishwa leo Mei 28, 2022 katika Uwanja wa Benjamin Jijini.
Isangi ameyasema hayo leo Mei 28 jioni baada ya kumalizika kwa mashindano hayo ambapo, ameeleza kuwa, katika mashindano mengine wanariadha wakipata kipindi kirefu cha kujiandaa watafanya vizuri zaidi na kuongeza viwango vyao kimataifa.
"Wito wangu kama mwanariadha nawashauri wanariadha kujituma kufanya mazoezi na kufuata maelekezo ya walimu wao ili waweze kutimiza ndoto zao kwa kuwa michezo kwa sasa ni ajira nani afya,"alisema Silas na kuongeza kwa kusema;
"Mchezo wa riadha ni moja ya michezo inayoleta sifa nchini kwahiyo wachezaji wetu waendelee kujituma ili tanzania tuendelee kung'ara kama kioo,"alisema.
Mashindano hayo yamefunguliwa na Naibu Waziri Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul na kufungwa na Kamishna wa Michezo Zanzibar Amir Mohamed Makame.
Timu ya Taifa ya Ethiopia katika mashindano hayo wamefanikiwa kutwaa ubingwa yalishirikisha nchi saba ambazo ni, Zanzibar, Ethiopia, Kenya, Eritrea, Sudan ya Kusini, Somalia na wenyeji Tanzania.
Tanzania imemaliza nafasi ya tano kwa kutwaa medali moja ya dhahabu, tatu za fedha na nne za shaba katika U -20 na timu ya U-18 wamekosa dhahabu na kuchukua fedha moja na tano za shaba.
Kwa upande wa Visiwani Zanzibar timu U-20 wamemaliza nafasi ya tatu kwa kuondoka na medali 2 za dhahabu, fedha 2 na shaba 1 na chini ya miaka 18 wamechukuwa nafasi ya 2 kwa kushinda medali 3 za dhahabu, 3 fedha na 2 shaba.
Timu ya vijana U 20 ya Kenya imemaliza nafasi 2 kwa kuondoka na medali 4 za dhahabu na 5 za fedha, kwa upande wa U-18 wakiwa nafasi ya tatu kwa kushinda medali 1 ya dhahabu, nne fedha na moja Shaba.
Eritrea imemaliza mashindano hayo wakiwa nafasi ya 4 kwa ujumla kwa upande wa timu ya U-20.