TANZANIA YAANZA VYEMA MASHINDANO YA BASEBALL 5 AFRIKA

Timu ya Taifa ya Tanzania ya mchezo wa Baseball imeanza vyema mashindano ya Baseball 5 Afrika kwa kuibuka na ushindi wa pointi 14 - 2 katika mzunguko wa kwanza na 4 - 1 katika mzunguko wa pili dhidi ya timu ya Taifa ya Zambia, mchezo uliochezwa katika uwanja wa ndani wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania Maclina Mutabuzi amesema chachu ya ushindi huo ni maandalizi ya muda mrefu na kufanya mazoezi kwa Bidii, ambapo lengo kuu ni kuhakikisha timu inafuzu kucheza mashindano ya Kombe la Dunia yatakayofanyika nchini Morocco.
"Tunashukuru tumeweza kufanya vizuri kwa sababu ya maandalizi ya muda mrefu tuliokaa kambini na kufanya mazoezi kwa bidii, wachezaji wetu wanajituma sana, na lengo letu kama timu ni kuhakikisha tunafuzu kucheza mashindano ya kombe la Dunia yatakayofanyika nchini Morocco", alisema Maclina
Naye Nahodha wa Timu ya Taifa ya Tanzania Adbul-Mounim Othman Ally amewaomba watanzania wajitokeze kwa wingi katika mashindano, kwa kuzingatia kuwa mashindano yanafanyika katika uwanja wa nyumbani lakini pia kuipa hamasa Timu ili iweze kufanya vizuri na kutwaa ubingwa wa mashindano hayo.
" nawaomba watanzania wajitokeze kwa wingi waje waishangilie timu yao inapocheza, sisi ndio wenyeji tupo nyumbani katika Ardhi yetu, tunaamini tutafanya vizuri na kuweza kulibakisha kombe nyumbani pamoja na kufuzu mashindano ya Dunia", alisema Adbul-Mounim.