WATANZANIA WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA CHAN

Watanzania wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu ya taifa ili kuipa hamasa na kuweza ya kufanya vizuri katika mashindano ya Fainali ya Mataifa ya Afrika wachezaji wa Ndani (CHAN) yatakayoanza Februari 1-28,2025 Kenya ,Uganda na Tanzania wakiwa wenyeji.
Akizungumza na waandishi wa Habari leo Januari 14,2025 jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya maandalizi ya mashindano ya CHAN na AFCON Leodegar Tenga, amesema watanzania wote hususani wapenzi wa michezo watumie fursa hii adhimu katika kuainisha fursa mbalimbali na kuzitumia ipasavyo.
"Watanzania wote mnaombwa kujitokeza kwa wingi wakati wa Mashindano kutoa hamasa kwa wanamichezo pamoja na kuchangamkia fursa mbalimbali katika mashindano hayo"amesema Tenga.
Aidha amesema kuwa wataomba kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) waweke viingilio vidogo na kuwe na utaratibu wa kuingia kw amani Ili mashabiki waweze kujitokeza wingi.
Akizungumzia miundombinu amesema Serikali inafanya maandalizi muhimu ikiwemo ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya mashindano hayo.
Amesema kuwa ukarabati unaendelea kufanyika katika uwanja wa Benjamini Mkapa na New Aman Zanzibar pamoja ujenzi wa viwanja vya mazoezi katika shule ya Sheria, Gymkhana na Meja Jenerali Isamuhyo.
"Viwanja hivi vitatumika kwenye mashindano ya chan na maandalizi ya miundombinu hiyo yamefikia asilimia 95,"alieleza.
Pia mwendelezo wa maandalizi upande wa hamasa limeandaliwa kongamano la wadau wa michezo litakalofanyika Januari 15, 2024 katika Ukumbi wa hoteli ya Rotana likilenga kutoa taarifa kwa wadau kuhusu hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya uenyeji na timu ya taifa sambamba na kupokea maoni, ushauri na mapendekezo kuelekea katika michuano hiyo.