TENGA AWATAKA VIONGOZI KUKIENDESHA KIKAO KWA TIJA
service image
27 May, 2022

Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Leodiger Tenga amefungua kikao kazi cha Viongozi wa Vyama/Mashirikisho na Kamati za michezo za Taifa huku akiwataka kukitendea haki kiwe na tija, kikao kinachofanyika leo tarehe 27 Mei, 2022 katika ukumbi wa Uwanja wa Benjamin Jijini Dar es salaam.

Tenga amesema kuwa kikao hicho ni utekelezaji wa maazimio yake kama Mwenyekiti na wajumbe wa Bodi ya BMT ya kuwa na vikao na vyama baada ya kuzinduliwa kwa bodi hiyo na Mhe. Waziri Mohamed Mchengerwa Waziri mwenye dhamana ya michezo mwezi machi.

Tenga amesema kikao hicho kina lengo la kujadili mafanikio na changamoto zilizopo katika vyama/mashirikisho na kamati za michezo ili kuwajengea uwezo wa nini wanatakiwa kufanya ili kuhakikisha michezo inaendelea nchini.

“Vikao kama hivi vinasaidia kutatua changamoto zilizokuwepo, matarajio yangu ni kuona kikao hicho kinakuwa na tija na kujadili na kuainisha viongozi nini tunatakiwa kufanya ili kufikia malengo yetu ya michezo kuwa imara na kuondoa changamoto zilizopo,” amesema Tenga.