CHANGALAWE AKIMCHAKAZA BINGWA MTETEZI SALAH KUTOKA MISRI.
service image
18 Mar, 2024

Kweli usiku wa Deni haukawii kukucha, ndivyo ilivyokuwa katika pambano la usiku wa kisasi katika ukumbi wa Bukom Arena, Accra - Ghana ambapo Nahodha wa Faru Weusi wa Ngorongoro  Yusuf Changalawe alitimiza ahadi yake ya kulipa kisasa kwa mpinzani wake Abdelgawwad Orabi Salah kutoka Misri kwa kumpiga kwa ushindi wa points.

Mkongwe huyo Salah alikuwa Bingwa mtetezi wa mashindano haya (akishinda Dhahabu Rabat 2019) na ndiye aliyemnyang'anya Changalawe tiketi mdomoni ya kufuzu Olimpiki ya Paris 2024 kwa Bara la Afrika katika uzani wa Light Heavyweight 80kg walipokutana katika pambano la fainali September 2023 katika uwanja wa Dakar Arena mjini Dakar, Senegal ambapo Salah aliibuka na ushindi wa points.

Changalawe alicheza pambano lake kwa ustadi wa hali ya juu sana na kusikiliza vizuri maelekezo ya walimu wake na kufanikiwa kumthibiti mpinzani wake huyo ambaye ameshafuzu kushiriki mashindano ya Olimpiki ya Paris 2024 ikiwa ni mara yake ya 2 kushiriki baada ya Tokyo 2020.

Katika hali ya kushangaza baada ya matokeo kutangazwa, Mmisri huyo alitumia muda mrefu kuduwaa ulingoni akiwa haamini kilichomtokea.

"Yes, it was pay back time, imetimia, nimewathibitishia naweza kuwa Bingwa Africa" Alisema Changalawe.

Sasa Changalawe atakutana na Bondia kutoka Equatorial Guinea katika hatua ya robo fainali ya mashindano ya Afrika Accra 2023.

Wakati huohuo Malkia Zulfa Macho alipoteza kwa points pambano lake la hatua ya robo fainali katika uzani wa Fly weight 52kg dhidi ya Gisele Nyembo kutoka DR Congo.