DKT. ABBASI: LENGO LIWE NI USHINDI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi ataka Ubunifu, weledi na ufanisi katika mkakati wa ushindi kwa michezo ya Jumuiya ya Madola inayotarajiwa kufanyika kuanzia Julai - Agosti, 2022 Birmigham nchini Uingereza.
Katibu Mkuu Abbas amesisitiza hayo kwa viongozi wa michezo itakakayoshiriki mashindano hayo.
"Ninachosema tunamalengo makubwa kuliko kipindi chochote kingine, tunachotaka ni kurudi na makombe tu," alisisitiza Katibu Mkuu.
Akiongea leo tarehe 28 Machi, 2022 wakati alipokutana na kamati ya maandalizi ya michezo hiyo ya Jumuiya ya Madola inayohusisha Serikali ikiwemo Wizara yenye dhamana ya michezo na Baraza la Michezo la Taifa pamoja na vyama vya michezo shiriki, ili kupokea ripoti ya maendeleo ya kambi tofauti za maandalizi ya timu kuelekea katika mashindano hayo.
Viongozi wa michezo shiriki ikiwemo mchezo wa riadha, Judo, ngumi, kuogelea na wanyanyua vitu vizito kwa watu wenye ulemavu wameeleza kuendelea vizuri na kambi za ndani lakini pia maandalizi yao ya kujipima katika mashindano ya ngazi ya kimataifa.
Dkt. Abbasi amewaondoa hofu viongozi wa michezo shiriki kuwa taarifa ya mawazo, maoni na ushauri wa kujenga ikiwasilishwa mapema ikiwemo makocha wa kigeni wenye viwango, kambi katika sehemu yenye hali sawia na sehemu ya mashindano na hata lishe bora kwa wachezaji, Serikali haitasita kuyafanyia kazi kwa lengo la mafanikio katika michezo hiyo.