DOKTA ABBASI APONGEZA KASI YA BMT KATIKA KUSIMAMIA SUALA LA UTAWALA BORA
service image
10 Feb, 2022

Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dokta Hassan Abbasi amelipongeza Baraza la MIchezo la Taifa (BMT), kwa kasi nzuri inayoendelea kufanya kwa kusimamia Utawala Bora hususani katika chaguzi za vyama vya michezo nchini.

Dkt. Abbasi ametoa pongezi hizo leo tarehe 10 Februari, 2022 alipokutana na Menejimenti ya BMT katika moja ya kumbi za uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Saaam, kujadili mambo muhimu ya kimkakati yanayotakiwa kuzingatiwa kwa sasa michezoni ikiwa ni pamoja na kusimamia maandalizi ya Timu za Taifa kuelekea katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.

“kwanza niwapongeze sana kwa kasi nzuri mliyonayo na mnayoendelea kufanya katika suala la kusimamia Utawala Bora hususani katika chaguzi za vyama vya michezo nchini, lakini pia tuna jukumu kubwa sana mbele yetu,kwanza kuangalia mambo ya kimkakati katika timu zetu za Taifa ikiwa ni pamoja na kusimamia maandalizi kuelekea katika mashindano mbalimbali ya kimataifa, kuna mashindano ya Jumuiya ya Madola, mashindano ya Dunia kwa mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu, hivyo ni vyema tukaanza maandalizi mapema kwa ajili ya kuziimarisha timu zetu ziweze kufanya vizuri,”amesema Dkt. Abbasi.

Aidha Dkt. Abbasi ameielekeza BMT pamoja na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini kuhakikisha wanafanya vikao na baadhi ya viongozi wa vyama na vilabu vya michezo, kwa lengo la kuendelea kuwakumbusha wajibu wao kwa mustakabali wa maendeleo ya michezo nchini.

“niwaagize BMT na Mkurugenzi, hakikisheni mnawaita na kufanya nao vikao baadhi ya viongozi wa vyama na vilabu vya michezo nchini, lengo ni kuendelea kuwakumbusha wajibu wao kwa mustakabali wa maendeleo ya michezo nchini na si vinginevyo, kama kuna mtu ambaye hataendana na kasi yetu basi hatuna budi kumuondoa ili tusirudi nyuma tulipotoka,”alisema Dkt. Abbasi.