Dkt. Biteko kufungua michezo ya 39 ya SHIMIWI jijini Mwanza
service image
07 Sep, 2025


Dkt. Biteko kufungua michezo ya 39 ya SHIMIWI jijini Mwanza

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko anatarajiwa kufungua rasmi michezo ya 39 ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala wa Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI) inayofanyika kwenye viwanja mbalimbali jijini Mwanza.

Mwenyekiti wa SHIMIWI, Bw. Daniel Mwalusamba amesema michezo itafunguliwa rasmi tarehe 07 Septemba, kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Michezo hiyo ilianza tarehe 01 Septemba, 2025 kwa hatua ya makundi ya mpira wa netiboli, mpira wa miguu, kuvuta kamba wanawake na wanaume, na hatua hiyo ilimalizika Septemba 5, 2025.

Bw. Mwalusamba amesema mwamko ni mkubwa kwa michezo ya mwaka huu ambapo hadi sasa takribani klabu wanachama 65 zinashiriki katika michezo mbalimbali.

Hatahivyo, amesema bado shirikisho linasisitiza kwa klabu ambazo zimeshindwa kushiriki michezo kwa mwaka huu zianze maandalizi kwa ajili ya michezo ya mwakani.

"Kama mnakumbuka Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo watumishi wa umma washiriki mazoezi na michezo ili kuimarisha afya zao, na bado tunaendelea kusisitiza kama kamati ya utendaji kuwa watumishi wa umma wanatakiwa kufanya mazoezi, basi kuangalia wakati wa bajeti kuweka mazingira mazuri ya kuwawezesha kushiriki,” amesema Bw. Mwalusamba.