JACKLINE SAKILU NA GABRIEL GEAY WANG'ARA MBIO ZA NYIKA TAIFA

Wanariadha Jackline Sakilu kwa upande wa wanawake na Gabriel Geay kwa upande wa wanaume, wamefanikiwa kushinda mbio za Nyika Taifa zilizofanyika leo tarehe 29 Januari, 2022 katika Shamba la Kahawa la Barku Jijini Arusha.
Jackline ametumia muda wa dakika 30:09:92 akifuatiwa na Maycelina Issa aliyemaliza nafasi ya pili kwa kutumia muda wa dakika 30:13:19 na nafasi ya tatu ikishikwa na Natalia Elisante aliyetumia dakika 30:16:27 katika mbio ya nyika kilomita 8.
Kwa upande wa wanaume Geay ametumia muda wa dakika 31:44:84 huku nafasi ya pili ikishikwa na Faraja Damas aliyetumia muda wa dakika 32:23:31 na nafasi ya tatu ikishikwa na Joseph Panga aliyetumia muda wa dakika 32:31:54.
Akizungumza mara baada ya mashindano hayo, Afisa Maendeleo ya Michezo (BMT) Abel Odena ameupongeza uongozi wa Riadha Tanzania kwa kuendelea kujiimarisha na kuandaa mashindano kwa ufanisi wa hali ya juu, lakini pia kutoa motisha kwa wachezaji kwa kuandaa zawadi nzuri zikiwemo medali na Fedha taslimu, ambapo mshindi wa Kwanza amepata shilingi laki tano (500,000), wa pili laki mbili na nusu (250,000), wa tatu laki mbili (200,000), wa nne laki moja na nusu (150,000) wa tano laki moja (100,000) na wa sita mpaka kumi (6-10) kila mmoja akipata shilingi elfu hamsini (50).