MAKOCHA NA WACHEZAJI WATAKIWA KUONGEZA BIDII KUIWEKA NCHI KATIKA USHINDANI WA JUU.
service image
26 Feb, 2022

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu amewataka wachezaji na makocha wa mchezo wa kuogelea kuongeza jitihada za kuifikisha nchi katika ushindani wa juu ili kufikia dhamira ya Mhe. Rais Samia Suluhu ya kuitangaza Tanzania kupitia michezo.

Bw. Yakubu amesema hayo Februari 26, 2022 wakati akifungua mashindano ya mchezo wa kuogelea yanayoratibiwa na Chama cha Waokoaji Tanzania (TALISS) ambapo mashindano hayo yanayofanyika kwa siku mbili katika shule ya Kimataifa ya Tanganyika jijini Dar es Salaam.

"Serikali inatambua na inaunga mkono jitihada zinazofanya na chama cha mchezo huu nchini pamoja na wadau wake katika kuuendeleza, lakini pia huu ni miongoni mwa michezo mikubwa duniani hatuna budi kujipanga kikamilifu kuhakikisha tunaundeleza" amesema Naibu Katibu Mkuu Yakubu na kuongeza kuwa,

"Nimepewa taarifa kuwa Tanzania tunaandaa mashindano ya kanda ya tatu (3) na tumealikwa Zambia mashindano ya kanda ya nne (4), mashindano haya ya TALISS yawe ni chachu ya kuchukua medali nyingi na makombe katika mashindano yote ambayo yapo mbele yetu" amesema Bw. Yakubu.

Aidha, Bw. Yakubu amewaeleza wadau wa mchezo huo  kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia inatambua changamoto iliyopo ya miundombinu ya michezo likiwemo bwawa la kimataifa la mchezo wa kuogelea ambapo amewahakikishia kuwa Serikali imetenga fedha ya kutosha kujenga  na kuboresha miundombinu hiyo, na bwawa ni moja ya vipaumbele hivyo.

Pia Bw. Yakubu katika hutoba yake amevisisitiza vyama na mashirikisho ya michezo nchini kuhakikisha wanaimarisha Utawala bora katika michezo ili kuwavutia wawekezaji kuiendeleza michezo nchini.

Hata hivyo amewaeleza wazazi kuwa Serikali inatambua mchango wao katika kuendeleza mchezo wa kuogelea huku akiwahakikishia kuwaa, iko  pamoja nao bega kwa bega kuona michezo inatangaza bendera ya nchi kimataifa. 

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mchezo wa Kuogelea Tanzania (TSA) Imani Dominick amewashukuru klabu ya TALISS pamoja na wadhamini wengine kufanikisha mashindano hayo.