MHE. MKANACHI: AITAKA TBF SHIRIKISHI
service image
31 Dec, 2021

Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Mheshimiwa Khamis Mkanachi amewataka viongozi wapya wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Nchini (TBF) kuyafanyia kazi maoni ya wanachama pamoja na wagombea ambao hawakuchaguliwa ili kulijenga na kuliimarisha Shirikisho hilo.

Hayo ameyasema jana tarehe 30 Disemba, 2021, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa Dodoma, Anthony Mtaka, baada ya kukamilika kwa uchaguzi wa viongozi wa shirikisho hilo ambao awali ulitanguliwa na Mkutano Mkuu wa Shirikikisho hilo uliofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Dear Mama jijini Dodoma.

"Chukueni maoni ya wengine na yawekeni kwenye mipango yenu ili muijenge na kuiimarisha TBF," alisema Mhe. Mkanachi.

Kwa upande wake Rais mpya wa TBF Michael Kadege amewahakikishia wanachama wa TBF waliomwamini kwa kumchagua kwa kura nyingi kuwa atashirikiana na watu wote ili kutimiza malengo yao hususani ya mpira wa kikapu kupiga hatua kubwa kimataifu

Viongozi wapya wa Shirikisho la Mpira wa kikapu nchini (TBF) kwa nafasi ya Rais ni Michael Kadege aliyeibuka kwa kura 52 dhidi ya mpinzani wake Phares Magesa aliyeambulia kura 08, nafasi ya Makamu wa Rais imeenda kwa Rwehabura Barongo kwa kura 44 dhidi ya wapinzani wake Mboka Mwambusi aliyeambulia kura 09 na Alphonce Kusekwa mwenye kura 07.

Nyingine ni nafasi ya Katibu Mkuu iliyochukuliwa na Mwenza Kabinda kwa kura 47 dhidi ya mpinzani wake Michael Mwita mwenye kura 13, nafasi ya Katibu Msaidizi imeenda kwa Benson Nyasebwa kwa kura 50 dhidi ya Daniel Kapoma mwenye kura 10, nafasi ya mwekahazina Leonard Haule mgombea pekee ameibuka na kura 54 za ndiyo na 06 za hapana.

Nafasi za Kamisheni ya Walemavu iliyokuwa na mgombea mmoja Azizi Mwaruka ameibuka na kura zote 60 za ndiyo, Kamisheni ya Watoto na maendeleo ya shule imeenda kwa Ramadhan Bakari kwa kura 29 dhidi ya Hamis Mpil aliyepata kura 26, Kamisheni ya Mipango na Maendeleo Fredrick Mtandu ameibuka mshindi kwa kura 39, Kamisheni ya Waamuzi mshindi ni Daniel Mbwana kwa kura 38 na Kmaisheni ya makocha Robert Manyerere mgombea pekee aliyeshinda kwa kura 46 za ndiyo.