MHE.SAMIA SULUHU HASSAN AFANYA MAKUBWA KATIKA TASNIA YA MICHEZO NDANI YA MWAKA MMOJA WA UONGOZI WAKE
service image
29 Mar, 2022

Waziri wa Utamaduni,Sanaa na Michezo Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa mambo makubwa aliyoyafanya katika Tasnia ya Michezo ndani ya mwaka mmoja wa uongozi wake wa awamu ya sita ikiwemo kutoa fedha katika mfuko wa maendeleo ya michezo kwa ajili ya kusaidia Timu za Taifa pamoja na miundombinu ya michezo nchini.

Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo leo tarehe 29 Machi, 2022 katika moja wa kumbi za uwanja wa Benjamin Mkapa alipokuwa anazungumza na wadau wa michezo waliojitokeza katika kongamano la michezo lililoandaliwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuelezea mafanikio ya michezo katika mwaka mmoja wa uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, ambapo amesema Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kuwekeza katika michezo ili kuendelea kufanya vizuri kitaifa na kimataifa.

Aidha Mheshimiwa Mchengerwa amewataka viongozi wa vyama vya michezo kujitafakari utendaji wao na kukemea vitendo vya baadhi ya viongozi wanaotumia vibaya nafasi walizonazo kujinufaisha wenyewe pamoja na kuhujumu maendeleo ya michezo wanayoisimamia.

“viongozi wenzangu niwaombe na kuwasihi sana,Mheshimiwa Rais ameendelea kutuamini, hivyo ni vyema tukaunga mkono juhudi alizozionyesha katika kutusimamia kwa ana nia njema ya kuendelea kuinua michezo yetu nchini,”amesema Mhe. Mchengerwa.

Lakini pia Mhe. Mchengerwa ametaja baadhi ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka mmoja wa Mhe. Samia ni pamoja na ongezeko la Bajeti katika tasnia ya michezo,ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya kisasa pamoja na uanzishwaji wa mfuko wa maendeleo ya michezo.