WAZIRI NDUMBARO AAGIZA KATIBU WA CHANETA KUHOJIWA NA KAMATI YA MAADILI BMT
service image
03 Mar, 2024

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro ametoa maelekezo kwa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kumwita Katibu wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta) Rose Mkisi na kutoa ushahidi wa tuhuma kwa serikali kwa kamati ya nidhamu ya BMT.

Maelekezo hayo ameyatoa leo Machi 03, 2024 wakati wa tukio la kuziaga timu za taifa zinazokwenda katika mashindano ya Afrika (All African Games) yanayotarajiwa kuanza Machi 8, 2024 jijini Accra, Ghana.

Aidha Waziri Ndumbaro amemwelekeza Mtendaji Mkuu BMT Bi. Neema Msitha kusitisha malipo yote kwa Chama hicho.

Dkt. Ndumbaro alisema amekasirishwa sana na maneno ya Katibu Mkuu wa CHANETA, Rose Mkisi kusema kuwa serikali haijali na kuthamini mchezo huo zaidi ya kuwekeza katika soka.

"Nawaagiza BMT kumuita Katibu wa CHANETA katika kamati ya nidhamu, pia aje na ushahidi wa tuhuma alizozisema katika mahojiano wakati anahojiwa na chombo cha habari," na kuongeza kwa kusema;

"Sitishe malipo yote hasa yale ya Afrika Kusini ambayo mlilipia tiketi, pia katika mkutano ambao nitafanya hivi karibuni na vyama na Mashirikisho Viongozi wa Chaneta wasiwepo hadi hili tatizo liishe, "alisema.

Katika hatua nyingine, Dkt. Ndumbaro amewataka wachezaji ambao wanashiriki mashindano ya Afrika kuhakikisha wanaenda kushindana na kupeperusha kwa ushindi bendera ya taifa na siyo kwenda kutalii.

"Nendeni mkapambane na kuleta heshima ya nchi kama klabu ya Simba na Yanga ambao wameweka historia kwa mara ya kwanza nchi kuingiza timu mbili katika robo fainali ya mashindano ya klabu Bingwa kwa msimu huu, "alisema.