MKUTANO MKUU WA KRIKETI WA AFRIKA ULIOFANYIKA HOTELI YA WHITESAND JIJINI DSM
service image
26 Apr, 2025

Katibu Mtendaji mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Neema Msitha amesema mafanikio ya Chama cha kriketi nchini yamekuwa chachu ya kufanikisha timu ya taifa ya vijana ya umri chini ya miaka19 kufuzu kushiriki mashindano ya kombe la Dunia yanayotarajiwa kufanyika Februari 2026 nchini Zimbabwe.

Msitha ameyanena hayo leo tarehe 25 Aprili, 2025 wakati akimwakilisha Naibu Waziri mwenye dhamana ya Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma katika ufunguzi wa mkutano mkuu wa kriketi wa Afrika unaofanyika katika Hoteli ya White Sand jijini Dar es salaam.

"Juhudi, uwajibikaji na uwazi kwa viongozi wa Chama cha Kriketi Tanzania (TCA) zimekuwa kivutio na kishawishi wa mchezo huo barani afrika,"alisema Msitha.

Naye, Mwenyekiti wa Baraza la Kriketi Duniani (ICC) Mubashshir Usman amesema mipango yao ni kuhakikisha mchezo huo Afrika unapiga hatua tofauti na miaka ya nyuma.

Mkutano huo wa afrika unafanyika Jijini Dar es Salaam kwa siku tatu ikiwa ni jukwaa la kujadili namna gani wachezaji wa Afrika katika mchezo huo wanafanya vizuri katika mashindano ya Dunia na kupanga mipango mipya ya kuuendeleza barani hapo.

Aidha, Katibu Msitha amewaeleza viongozi hao wa mchezo wa kriketi Afrika na Duniani wasisite kuja kufanyia mikutano yao Tanzania kwakuwa ni sehemu salama yenye amani na vivutio tofauti na kuongeza kuwa hawajutia.