MSITHA AWATAKA WAAMUZI KUTUNZA LADHA YA SOKA
Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Neema Msitha amewataka waamuzi kutunza ladha ya mpira wa miguu.
"Hii ladha ndio inatusaidia kupata fedha kutoka kwa wafadhili tofauti lakini pia inasaidia kupeleka mbele ajenda za serikali kupitia michezo, nyie mnaweza kutengeneza au kuharibu na mkiharibu mnafukuza wafadhili,"alisema Msitha na kuongeza kuwa:
"Tunaihitaji hii michezo kwakuwa ndiyo ajira yetu na wote tunategemeana, na katika kutegemeana mmoja asimwangushe mwingine," alisisitiza.
Hayo ameyasema leo tarehe 15 Februari, 2022 wakati akifungua kozi ya Waamuzi wa soka inayoratibiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) pamoja na Bodi ya ligi inayofanyika kwa siku tatu (3) kuanzia tarehe 15 hadi 17 Februari, 2022 katika moja ya kumbi za Uwanja wa Benjamin Jijini Dar es salaam.
Aliendelea kwa kuwataka waamuzi hao kulinda taaluma yao kwa kuwathibitishia Watanzania na jamii ya Waafrika ambao wanajua michezo ni mzaha kwa kujitofautisha na wasiokuwa na taaluma hiyo.
Aidha Msitha amewasisitiza waamuzi hao kulinda haki ya wachezaji na timu na kueleza kuwa, Mtu anapofungwa katika mazingira ya haki hawezi kulalamika.
Hatahivyo Msitha amewataka TFF katika kozi wanazoendesha kuona umuhimu wa kuwaleta wataalamu wa Taasisi ya kupambana Rushwa ili waamuzi wapewe elimu kuhusu rushwa.
Kwa upande wa mmoja wa waamuzi wa kozi hiyo Ally Sasii amewashukuru TFF na bodi ya ligi kwa kuandaa kozi hiyo ambayo itaendelea kuwakumbusha na kuwaongezea ujuzi na amewaahidi watanzania kuwa wataendelea kufanya kazi hiyo kwa weledi na kutenda haki.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi Nassor Hamid ameeleza kuwa kozi hizo ni mwendelezo kozi za mara kwa mara ili kuwakumbusha waamuzi dhamana yao kwa jamii na wachezaji lakini pia kuendana na wakati kwakuwa kila siku mambo yanabadilika.