TUZO ZA BMT 2023
service image
15 May, 2024

BMT kutoa tuzo kwa Wanamichezo Bora Juni 09, 2024.

Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limeandaa tuzo za wanamichezo bora wa mwaka 2023 waliofanya vizuri katika mashindano ya Kimataifa tukio litalofanyika Juni 9,2024 kwenye Ukumbi wa The super Dome jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa Habari leo Mei 15, 2024 jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Kamati ya tuzo za BMT Profesa Madundo Mtambo, alisema kuwa lengo ni kuwatambua na kuwaenzi wanamichezo na timu za Taifa zolizofanya vizuri katika mashindano ya Kimataifa.

Alisema kuwa mchakato wa utoaji tuzo unafanyika kwa uwazi, weledi, na umakini mkubwa kwani Baraza limeshirikisha vyama na mashirikisho yote ya michezo katika uteuzi wa wanamichezo bora katika michezo yao. Kamati ya usimamizi wa tuzo imepokea mapendekezo ya vyama, itayachambua na kuchagua wanamichezo bora.

"Mabadiliko ya vipengele vya tuzo yamefanyika ili kuendelea kuzipa thamani tuzo hizi zinazotolewa pamoja na kuongeza ushindani baina ya wanamichezo ili mwanamichezo anayepewa tuzo awe ni yule ambaye amekuwa na mafanikio zaidi kuliko wanamichezo wengine wote," alisema Profesa Mtambo.

Alibainisha kuwa Kamati ya usimamizi itafanya Kwa ukaribu na vyama vya michezo vya kitaifa katika kutambua washindi wa vipengele mbalimbali vya tuzo na kutambua timu na wanamichezo waliofanya vizuri na kupitiwa na sekretarieti na baadaye itathibitishwa na Kamati hiyo.

Prof. Madundo ametoa wito kwa wadau mbalimbali yakiwamo makampuni ,Taasisi za Serikali na binafsi na watu mmoja mmoja wanaopenda maendeleo ya michezo nchini kujitokeza kuipa nguvu BMT katika kutekeleza jukumu hilo la faraja kwa Wanamichezo.