Ngome mabingwa wa klabu bingwa ngumi Taifa 2025
Timu ya Ngome inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) imefanikiwa kutwaa Ubingwa katika mashindano la Klabu Bingwa ya Taifa Tanga 2025, Septemba 20, 2025 katika uwanja wa michezo wa Urithi, Jijini Tanga baada ya kuibuka na medali sita za Dhahabu dhidi ya nne za MMJKT aliyeshika nafasi ya pili huku Magereza wakishika nafasi ya tatu na Jeba boxing akishika nafasi ya nne.
Jumla ya vilabu 9 kati ya 15 vilifanikiwa kupata medali katika mashindano hayo na zawadi za vikombe zikitolewa kwa wachezaji bora na anayechipukia, mwalimu bora, mwamuzi na jaji bora na timu yenye nidhamu.
Mchezaji wa bora wa kiume alichukua Faki Issa kutoka timu ya Jeba Boxing ya Tanga na kwa wanawake ilichukuliwa na Zainabu Kutaka kutoka MMJKT huku mchezaji anayechipukia ikichukuliwa na Issa Shabani kutoka Ngamiani ya Tanga.
Mwalimu bora wa mashindano hayo ilichukuliwa na Mzonge Hassan Mraba kutoka Ngome wakati Mwamuzi na Jaji bora ikichukuliwa na Saidi Hofu.
Timu yenye nidhamu bora ilichukuliwa na timu ya Magereza waliorudi vizuri kwenye ramani ya mchezo wa ngumi nchini, chini ya mwalimu mkuu wao IBA 1 Star Coach Athony Kameda.
Moja ya mapambano ya fainali ya kuvutia yalikua kati ya mchezaji bora wa mashindano Faki Issa kutoka Jeba Boxing alipoweza kumsimamisha Maope Joseph kutoka MMJKT katika round ya 2 katika uzani wa featherweight 57kg huku Saidi Mtibala (Ngome) akishinda kwa 3-2 dhidi ya Iddi Athumani kutoka MMJKT.
Bondia wa viwango Alphonce Abel kutoka MMJKT alifanikiwa kuibuka na ushindi wa KO round ya 2 dhidi ya Milumbe James kutoka Ngome.
Kwa upande wa wanawake uzani wa light flyweight 50kg Star Princess Asha Iddi aliibuka kwa ushindi wa points 3-2 dhidi Marther Patrick wa Ngome aliyempa upinzani mkali huku katika uzani wa bantamweight 54kg Star Lady Zainabu Kutaka wa MMJKT akishinda kwa points 5-0 dhidi ya Vumilia Twalibu wa Ngome.

